Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

REA YAPELEKA UMEME VITONGOJI 120 KIGOMA


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye majimbo 15 ya Mkoa wa Kigoma ambao utawezesha jumla ya vitongoji 120 kupata umeme wa uhakika utakaowarahisishia kufanya shughuli za kiuchumi na kujenga Taifa.

Hayo yemebainishwa leo Oktoba 16, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye mara baada ya kupokea taarifa ya REA kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa miradi hiyo ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 120 mkoani humo.

"Nawapongeza REA kwa kutekeleza mradi huu wa kupeleka umeme kwenye vitongoji. Umeme ni chachu ya maendeleo katika mkoa huu kwani unategemewa katika shughuli za kiuchumi na kijamii," Ameongeza Mhe. Andengenye.

Mhe. Andengenye ameitaka Kampuni ya Routeways Technologies Ltd inayotekeleza miradi hiyo kuhakikisha inaukamilisha mradi kwa wakati katika kipindi kilichopangwa katika makubaliano yao.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya REA kanda ya Magharibi, Mha. Robert Dulle amesema wamemtambulisha mkandarasi huyo ambaye atatekeleza miradi ya vitongoji 15 kwa kila jimbo la uchaguzi katika mkoa wa Kigoma.

"Mkandarasi huyu anajulikana kwa jina la Routeways Technologies Ltd anatekeleza mradi huu katika vitongoji 15 kila jimbo kwa gharama ya shilingi bilioni 14 ambazo fedha zote zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili wananchi wa Kigoma wapate umeme." Amesema Mha. Dulle.

Ameongeza kuwa, mradi huo ulianza mwezi Agosti mwaka huu ambapo utatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka 2026.
Katika hatua nyingine, mkandarasi wa miradi hiyo ameelekezwa kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wa Kigoma wanufaike na nishati ya umeme katika vitongoji hivyo.

Naye, Mhandisi John Odhiambo, wa kampuni ya Routeways Technologies Ltd inayotekeleza miradi hiyo amesema watahakikisha mradi unakamilika kwa haraka katika kipindi kilichopangwa ili kuwawezesha wananchi wa maeneno hayo kupata nishati hiyo muhimu.

Mkandarasi yupo katika hatua za awali za kukamilisha taratibu za kuanza kazi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com