RUSHWA SI UTAMADUNI WA MTANZANIA:SHEKIMWERI




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Sauti ya wapinga rushwa ya "Anti Corruption Voices" ya Jijini hapa imesema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali kuipinga rushwa bado kuna haja ya kuendelea kuelimisha Jamii namna ya kuepukana na rushwa ya ngono.

Taasisi hiyo ambayo imebeba ajenda ya kupinga vitendo vya rushwa kwenye jamii imesema rushwa si sehemu ya utamaduni wa mtanzania na hivyo Jamii nzima inapaswa kuikataa kwani inadhalilisha utu wa mtu.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 7,2024 Jijini hapa na Mwenyekiti wa bodi ya Kampeni ya Sepesha rushwa Dina Daniel inayoendeshwa na Taasisi hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa msimu wa mbio za Marathon kwa mwaka 2024.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Rushwa ya ngono bado inanuka huku akitolea mfano kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wakiwa kwenye siku za wanakatwa mshahara siku zote wanazokaa nyumbani.

"Rushwa ni adui wa haki inadhalilisha utu wa mtu, imefikia hatua baadhi ya wanawake wanapokuwa kwenye siku zao wanakata mshahara kufidia zile siku ambazo walishindwa kumudu kutokana na maumivu, adhabu hii ni unyanyasaji na tunaiita rushwa, " amefafanua

Kuhusu kuanza kwa msimu wa mbio za marathoni zilizopewa jina la "Sepesha Rushwa" na kupewa kauli mbiu ya "Acha Rushwa ya Ngono" zinaenda kumaliza rushwa kwenye jamii na kueleza kuwa kwa awamu hii nguvu inaelelezwa kwa vijana ambapo itawaelimisha namna ya kuondokana na rushwa ya ngono na kuepukana na rushwa hiyo .

"Rushwa imekuwa ni tatizo kwenye jamii, Mwalimu nyerere aliliona tangu Zaman akasema rushwa ni adui wa haki,tuitangazie dunai kuwa rushwa inakosesha uhalali wa huduma na kufifisha ndoto za watu,kuna haja ya kuelimishana na kukumbushana namna ya kuwajibika," ameeleza

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh.Jabir Shekimweri ameeleza kufurahishwa kwake kwa namna ambavyo Taasisi hiyo inafanya kazi ya kuelimisha jamii kuepuka vitendo vya rushwa na kueleza kuwa Mapambano ya rushwa yanapaswa kuwa endelevu.

"Jamii inapoikumbatia rushwa inasababisha kudhuru mifumu ya haki na usawa,kwa pamoja nitashirikiana nanyi kuibeba ajenda ya sepesha rushwa marathon 2024 kuhakikisha rushwa ya ngono vyuoni na sehemu nyinginezo inatokomezwa, " ameeleza

kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Hazina Eugene amesema wamekuwa wakishirikiana na jamii katika kuhakikisha wanapiga vita adau mkubwa rushwa ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wameweza kushughulikia kesi mbalimbali.

" Rushwa ni adui wa haki hivyo ni vyema jamii kutambua na kuacha kutoa na kupokea rushwa ya aina yoyota, " Amesema Mwakilishi huyo wa TAKUKURU

Pamoja na Mambo mengine Kampeni hiyo itatumia miezi miwili kuelimisha jamii kuanzia Oktoba hadi Desemba ambapo jumla ya Washiriki 5000 watahudhuria lengo likiwa ni kusambaza elimu ya rushwa ya ngono na kuwa sehemu ya mabalozi kwa jamii kwa ujumla.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post