Na Dotto Kwilasa,Dodoma
SERIKALI kwa mwaka wa fedha 2024/2025, imetenga jumla ya Sh. bilioni 14, kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 544 kwa mafunzo ya Ubingwa na Ubingwa bobezi pamoja na wataalamu wengine 47 kwa utaratibu wa seti.
Fedha hii ni ongezeko la Sh. bilioni 3.05 sawa na asilimia 28 zaidi ya bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya Sh. bilioni 10.95 kwa mwaka.
Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amebainisha hayo leo October 21 jijini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mpango huo wa serikali kusomesha wataalamu bingwa na wabobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha.
“Katika kufanikisha azma ya kuwa na watalaamu wenye ujuzi wa kutosha wa kutoa huduma bora za matibabu hapa nchini, Wizara ya Afya ilijiwekea lengo la miaka mitano (2020-2025) la kusomesha wataalamu bingwa na wabobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha. Kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Serikali unaojulikana kama ‘Samia Health Specialization Scholarship Program”alisema Mhagama
Amesema wataalamu 829 wanaoendelea na masomo ya ubingwa na ubobezi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi wataendelea kupewa ufadhili kupitia fedha hizo.
Vile vile, amesema kwa mwaka huu wa fedha Wizara ilipokea jumla ya maombi ya ufadhili 948 nchi nzima, kati ya hao waombaji wa jinsia ya kike ni 353 sawa na asilimia 37 na ya kiume ni 595 sawa na asilimia 63.
"Yote haya ni kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Samia Health Specialization Scholarship Program ambao utafanikisha kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi na hivyo kupunguza gharama kwa serikali na wananchi pamoja na kuvutia tiba utalii, amesema na kuongeza;
"Kati ya hao, waombaji 771 walikidhi vigezo vya kufadhiliwa na waliochaguliwa kwa ajili ya ufadhili ni 544 sawa na asilimia 71 ya waombaji waliokidhi vigezo, kati ya watumishi 544 waliochaguliwa kupata ufadhili, jinsia ya kiume ni 338 sawa na asilimia 62 na jinsia ya kike ni 206 sawa na asilimia 38,"anafafanua
Amesema watumishi waliochaguliwa kupata ufadhili katika vyuo vya ndani ya nchi ni 517 sawa na asilimia 95 na nje ya nchi 27 sawa na asilimia tano.
“Kwa takwimu hizi, kumekuwa na ongezeko la kufadhili watumishi wanaoomba kusomeshwa na serikali kutoka asilimia 56 mwaka 2022/2023 hadi asilimia 71 mwaka 2024/2025.
“Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya Afya imeshatumia jumla ya shilingi bilioni 30.95 katika kuendeleza wataalamu bingwa na bobezi katika sekta ya afya nchini”alisema
Amesema, Wizara imezingatia vipaumbele muhimu vya kisekta kama ubobezi katika ngazi mbalimbali za huduma pamoja vipaumbele kama vilivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa tano wa Sekta ya Afya pamoja na bajeti ya Wizara ya mwaka 2024/25.
Social Plugin