Serikali inakuja na mpango wa kuongeza misitu ya asili kwa kila Halmashauri nchini kuwa na msitu wake ikiwa moja ya njia ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira ambapo baadae itasaidia kwenye biashara ya kaboni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo Oktoba 23,2024 mkoani Tanga wa ziara yake ya kikazi ya kukagua, kufugua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Kijaji ameeleza kuwa lengo ni halmashauri hizo kuingia kwenye biashara ya Kaboni ambapo zoezi la kupandwa miti kwa pamoja kutawezesha faida kuonekana haraka kuliko kupandwa na mtu mmoja mmoja.
Waziri Kijaji ameongeza , mpango huo utashirikisha hasa wale ambao wana maeneo makubwa ya ardhi ambapo wanaweza kutumia ekari tano mpaka kumi kwa ajili ya kupanda miti hiyo.
“Kufanikiwa kwa kupandwa miti hiyo kutasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo mengine yanasababisha ongezeko la joto pamoja na mvua ambazo hazina mpangilio mzuri.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kumekuwepo changamoto ya wananchi kuchoma misitu hovyo na hivyo wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuona jinsi ya kuzuia matukio hayo.
Ameongeza kuwa mkoa huo una zaidi ya hekta laki saba za misitu ambapo ndani yake kuna mashamba matatu ya miti lakini kumekuwa na changamoto ya wananchi kuvamia na kuingiza mifugo pamoja na kuchoma mkaa, na mamlaka husika zinaendelea na udhibiti.
Amesisitiza kuwa katika mkoa huo wananchi pia wamekuwa wakijishuhurisha na kilimo cha mikokoo ambacho kinasaidia katika utunzaji wa mazingira ya bahari kwani wakati wa mmomonyoko wa udongo miti hiyo inasaidia kusitokee uharibifu kwenye maeneo ambapo mikoko ipo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akiongea na Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Bw. Selemani Sankwa mara baada ya kusaini kitabu cha wageni. Waziri Mhe. Dkt. Kijaji anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kuanzia Oktoba 23,2024 ambapo anatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya kuongea na wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisaini kitabu cha wageni Ofisi ya Mkoa wa Tanga mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Oktoba 23,2024 ambapo anatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya kuongea na wananchi mkoani humo.
Social Plugin