Na Mwandishi wetu, Geita
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko ameupongeza Mgodi wa Anglo Gold Ashanti kwa kujenga nyumba sita za makazi ya Maafisa wa Jeshi la Polisi.
Katika mkakati wa kutambua kazi nzuri wanazofanya Maafisa hao katika jamii, sambamba na kuwapa motisha katika majukumu yao ya kulinda nchi na usalama wa raia.
Biteko aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo, uliofanyika mkoani Geita leo 5, Oktoba 2024. Ambapo alisisitiza umuhimu wa Maafisa wa Jeshi la Polisi kuendelea kutenda haki na kufanya kazi kwa weledi ili kulinda usalama wa raia na mali zao.
"Ukiona tunalala salama, tunaamka salama pamoja na mali zetu, kuna kundi dogo sana la watu ambao hawasinzii hata kidogo ili sisi wote tuendelee kuwa salama," amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, alieleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa Jeshi hilo katika kujenga mazingira bora na kuboresha utendaji kazi.
Alitoa wito kwa sekta ya Madini na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Jeshi la Polisi katika miradi ya kimkakati ili kuimarisha mifumo ya usalama wa raia na mali zao, na kutunza amani na utulivu wa nchi.
Makamu wa Rais wa Mgodi wa Aglo Gold Ashanti, Simon Shayo alibainisha sababu ya kuwajengea nyumba za kisasa Maafisa wa Jeshi hilo kuwa "huwezi kuwa na mgodi ambao ni salama kama jamii inayokuzunguka haipo salama."
Alieleza kuwa miradi hiyo ya kwawajengea nyumba Maafisa wa Jeshi la Polisi ilianzishwa mwaka 2019 kama sehemu ya kuimarisha makazi ya viongozi wa Jeshi hilo mkoani Geita, na unalenga kuboresha usalama katika eneo hilo.