Na Oscar Assenga,HANDENI.
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu yaliyotokea Septemba 23 mwaka huu katika eneo la ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Korogwe Kijiji Kata ya Sindeni wilayani Handeni mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga (ACP) Almachius Mchunguzi ambapo alisema kwamba katika tukio hilo gari aina ya Toyota IST yenye namba T.305 EAL ambapo ndani na nje ya gari hilo iligundulika miili ya watu watatu.
Katika miili hiyo ya watu watatu iligundulika pia mwili wa aliyekuwa Mkaguzi wa Ndani (Internal Oditor wa Halmashauri ya Korogwe wilaya Bi Jonais Edward Shayo (46) na mtoto wake Dedani Lameck Shayo (8) na Salha Bakari Hassani (Dada wa Kazi) (18) Mkazi wa Bagamoyo wilaya ya Korogwe.
“Miili hiyo ilibainika kuwa ni ya watu hao baada ya kufanyika utambuzi na uchunguzi wa kitaalamu”Alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga.
Alisema kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi na msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita ambap ni Benard Adam Kizughuto (31) mkulima na mkazi wa Msambiazi wilaya ya Korogwe, Marko John Jambia Rajabu Mhilu(28) mkulima mkazi wa Lushoto,Peter John Jambia Johson (31) mkulima mkazi wa Msambiazi Korogwe.
Aliwataja wengine kuwa ni Hassani Ramadhani Bakari Kitombo Jombi (53) mkulima na mkazi wa Kwamaraha wilaya ya Handeni,James Mkama Teacher (42) mfanyabiashara na mkazi wa Mtonga wilaya ya Korogwe na Omari Saleh Mwiba (20) mkulima na mkazi wa Kwamaraha wilaya ya Handeni.
Kamanda Mchunguzi alisema kwamba upelelezi wa shauri hilo unaendelea kukamilishwa ili hatua nyengine za kisheria zifuate
Hata hivyo alisema kwamba Jeshi hilo linalaani vikali vitendo vyote vya kihalifu na halitomuonea muhali wala halitasita kuwachukulia hatua za kisheria mtu yeyote au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitend vya kihalifu.
“Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushrikiana na Jeshi la Polisi katika kubaini na kuzuia uhalifu ili kuendelea kuuweka mkoa wetu salama”Alisema
Social Plugin