TANZANIA YANG'ARA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAJARIBIO WA BIASHARA AFCFTA

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) akisalimiana na Mhe. Prof.Margaret Kamar kutoka Kenya ambaye ameongoza Ujumbe wa Kamati ya Bunge La  Afrika kuhusu Utafiti na Utetezi katika Masuala ya Biashara, Forodha na Uhamiaji katika Utekelezaji wa Mpango wa Majaribio ya ufanyaji biashara chini ya Mkataba wa AFCFTA Tanzania katika kikao kilichofanyika Oktoba 22, 2024 Bungeni Jijini Dodoma.

..........

Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema Utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) nchini Tanzania umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji katika miundombinu muhimu kama vile Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Barabara, ununuzi wa ndege za abiria na mizigo na marekebisho ya Sheria na Sera za biashara iliyolenga kuboresha usafirishaji wa bidhaa usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi, kupunguza gharama, kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko la Afrika na kufaidika kikamilifu na fursa zinazotolewa na AfCFTA."

Ameyasema hayo Oktoba 22, 2024 alipokuwa akiongea na Ujumbe wa Kamati ya Bunge La  Afrika kuhusu Utafiti na Utetezi katika Masuala ya Biashara, Forodha na Uhamiaji katika Utekelezaji wa Mpango wa Majaribio ya ufanyaji biashara chini ya Mkataba wa AFCFTA Tanzania katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Akijibu maswali ya ujumbe huo uliojumuisha Wabunge wa Bunge hilo kutoka Kenya pamoja na wajumbe wengine kutoka Tanzania, Afrika ya Kato, Seychelles, Morocco, Benin na Gabon amesema Tanzania imeendelea kutekeleza Mpango huo kwa mafanikio kutokana na jitihada mbalimbali zinazolenga kuboresha Mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za biashara na kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiushuru baina ya nchi na kikanda ambapo Tanzania ni mwanachama.

Aidha, amebainisha kuwa Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi nane (8) za mwanzo zilizopewa kipaumbele cha kupeleka bidhaa 10 kuanzia julai 2023, jumla ya Kampuni 11 zimeweza kuuza bidhaa zake katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kutumia cheti cha uasili wa bidhaa cha AfCFTA ambapo, jumla ya vyeti 24 vimeweza kutolewa kwa Kampuni hizo. Bidhaa ambazo zimeuzwa kwa wingi kupitia vyeti hivyo ni nyuzi za katani tani 426.4 kwenda nchi za Nigeria, Ghana, Morocco na Misri, kahawa tani 273.3 kwenda nchini Algeria na tumbaku tani 21.1 kwenda Nigeria.

Vilevile, Dkt. Jafo ameeleza kuwa Wizara yake inaendelea kutoa mafunzo na kuwahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo kwa kuuza bidhaa zenye ubora na uasili wa Tanzania kulingana na mahitaji ya soko hilo linalojumisha Nchi 54 za Afrika, kwa kuwa AfCFTA inatoa fursa ya kuuza bidhaa au huduma ndani ya Bara la Afrika bila vikwazo vyovyote visivyo vya kiushuru kwa Nchi yoyote Afrika ambayo ni Mwanachama bali kwa kutozwa ushuru pungufu ikilinganishwa na ilivyokuwa awali. Akiongoza ujumbe wa kamati hiyo, Mhe. Prof Margaret Kamar kutoka Kenya amesema Tanzania ni mfano mzuri katika utekelzaji wa mpango huo kwa kuwa ni Mwanachama hai wa jumuiya za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na Soko la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) zilizopo ndani ya Afrika na ina uzoefu wa kufanya biashara na kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara zinazojitokeza katika jumuiya hizo

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) akisalimiana na Mhe. Prof.Margaret Kamar kutoka Kenya ambaye ameongoza Ujumbe wa Kamati ya Bunge La Afrika kuhusu Utafiti na Utetezi katika Masuala ya Biashara, Forodha na Uhamiaji katika Utekelezaji wa Mpango wa Majaribio ya ufanyaji biashara chini ya Mkataba wa AFCFTA Tanzania katika kikao kilichofanyika Oktoba 22, 2024 Bungeni Jijini Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post