Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YARIDHISHWA NA USHIRIKIANO ULIOPO NA NCHI YA NAMIBIA




Na Mwandishi wetu, NAMIBIA

Tanzania itaendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wa diplomasia baina yake na nchi ya Namibia katika kuimarisha mahusiano yaliyopo katika nyanja mbalimbali huku mchango wa Tanzania katika uhuru wa Namibia ukitajwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga mapema 24 Oktoba, 2024 alipotembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia, ambapo aliambatana na watendaji wa ofisi hiyo kwa lengo la kushiki Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa pamoja na Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na vitakavyofanyika Windhoek nchini Namibia. Mikutano hiyo itafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2024.

Mhe. Ummy ameeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uongozi makini, na mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyojipambanua kidiplomasia na kuhakikisha mahusiano ya Taifa na nchi nyingine unakuwa wenye manufaa na kuiletea nchi heshima katika nyanja mbalimbali.
“Hakika Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha amani na utulivu, hii imetokana na uongozi mahiri wa Mhe.Rais Dkt. Samia kwa miongozo na maelekezo yake katika kuhakikisha nchi inaendelea kujipatia maendeleo,”amesema Mhe. Ummy

Aidha, katika mazungumzo na mwenyeji wake ambaye ni Afisa Mambo ya Nje Mkuu na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Namibia Bw. Elias Tamba ameeleza kuwa, nchi ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Namibia katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia urafiki uliopo baina ya Mataifa hayo mawili toka kipindi ya Uhuru wa Namibia ambapo Tanzania inakumbukwa kwa mchango wake.

Bw. Tamba ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuhakikisha inaimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina yake na Namibia huku akizitaja fursa za kimaendeleo kwa taifa hilo ikiwemo masuala ya kibiashara.

Ujumbe wa Tanzania nchini Namibia umeongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga akiwa ameambatana na Timu yake kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu akiwemo Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt.Jim Yonazi, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi hiyo Brig. Jenerali Hosea Ndagala, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo pamoja na Bw. January Kitunsi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi mara baada ya kikao katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania Nchini Namibia.















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com