Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAWA YAANZA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA RAIS SAMIA MIKOA YA RUVUMA NA LINDI

 


Na Beatus Maganja, Ruvuma


Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema kufuatia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo inayowakabili wananchi hasa katika mikoa ya Ruvuma na Lindi, Serikali kupitia TAWA imetenga bajeti kwa ajili ya kununua ndege nyuki nne (4) aina ya DJI Mavic 3 ambazo zitapelekwa katika wilaya za Namtumbo (Ruvuma) na Liwale, Nachingwea na Lindi mkoani Lindi.


Kamishna Mabula ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2024  mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati wa ziara ya kufuatilia utakelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa Mkoani humo  Septemba 28, 2024  kuhusu udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.


Sambamba na hilo, Mabula amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 TAWA inatarajia kuajiri Askari 351 ambao watapangiwa vituo vilivyopo kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyamapori hao ambapo Askari 20 watapangiwa katika kituo kidogo cha Songea na watafanya kazi katika wilaya za Tunduru na Namtumbo, wilaya zinazotajwa kuwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.


Vilevile, Kamishna Mabula amesisitiza kuwa TAWA inatarajia kununua gari moja (1) na pikipiki mbili (2) ambavyo vitapelekwa kituo kidogo cha Songea na vitatumika Katika kudhibiti changamoto ya wanyamapori hao katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.


Pia, Mamlaka itaboresha kituo kimoja cha Askari cha kudumu katika wilaya ya Tunduru na vikosi viwili vya kudumu vya Askari kutokea kituo kidogo cha Songea ili kurahisisha mwitikio wa haraka wa matukio ya tembo.


Kamishna Mabula ameongeza kusema kuwa baada ya changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuendelea kuonekana inakuwa kubwa, Wizara ya Maliasili na Utalii iliandaa Mkakati wa kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu ambao unatekelezwa na Taasisi za Wizara zilizo chini ya Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (TAWA , TANAPA, NCAA na TFS) kwa kugawana maeneo, Halmashauri za Wilaya, Taasisi zisizo za kiserikali, wadau wa Uhifadhi na wananchi kwa ujumla


Aidha, katika hatua nyingine kutokana na uwepo wa bustani ya wanyamapori hai inayosimamiwa na TAWA (Ruhila Zoo) katika Manispaa ya Songea, bustani inayotajwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa wakazi wa Mkoa huo, Kamishna Mabula amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed kusaidia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 5 ambayo itafika moja kwa moja katika bustani hiyo ili kuwawezesha wakazi wa Mkoa huo kufika kirahisi katika kivutio hicho cha utalii.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amempongeza Kamishna huyo kwa hatua za haraka alizochukua za kufuatilia utakelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia maelekezo aliyoyatoa alipokuwa katika ziara yake mkoani humo mwezi Septemba, 2024.


Kanali Ahmed Abbas Ahmed pia ameipongeza TAWA kwa jitihada walizochukua kama mipango ya muda mfupi na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto hiyo mkoani humo na kukiri kuwa jitihada hizo zinarudisha matumaini kwa wananchi wa Ruvuma kwa kuwa zinalenga kuimarisha usalama wa maisha na mali zao dhidi ya uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo ya wananchi hao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com