Na. Beatus Maganja
Maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini - TAWA kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Kahunda kilichopo Kata ya Katwe Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema na mkoa wa Mwanza wamefanikiwa kumdhibiti mamba aliyezua taharuki takribani wiki nzima Kijijini humo kabla ya kuleta madhara Kwa binadamu.
Tukio la kumdhibiti mnyama huyo mkali na mharibifu lilitokea oktoba 03, 2024 mara baada ya wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa Maofisa wa TAWA Kanda ya ziwa kituo kidogo cha Mwanza ambao walifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumdhibiti mnyama huyo Kwa kumuua Kwa mujibu wa Sheria.
Wananchi wa Kahunda wamesema mamba huyo amekuwa akileta taharuki takribani wiki nzima Kwa kukamata mifugo yao wakiwemo bata, kuku na mbwa Katika mwalo wa Kijiji hicho na Kijiji cha zabaga hali ambayo ilikuwa ikiwafanya waishi Kwa wasiwasi mkubwa na kushindwa kufanya shughuli za kibinadamu Kwa amani katika ziwa hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kahunda Bw. Athumani Wambura ameipongeza Serikali kupitia maofisa wa TAWA kwa kufanikisha zoezi la kumdhibiti mamba huyo na jitihada zote zinazofanywa na taasisi hiyo Kijijini humo ikiwa ni pamoja na hatua mbalimbali wanazochukua Katika kulinda maisha ya wananchi wa wilaya ya Sengerema dhidi ya athari za wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko.
"Niseme tu nawapongezeni sana hawa ndugu zangu wa maliasili (TAWA) jambo walilolifanya ni kubwa kwa wananchi wetu, Kwa namna moja au nyingine tumepata amani kwa kumdhibiti huyu mnyama ambaye ni tishio kubwa sana. Kwa miaka ya hivi karibuni wanyama hawa wameweza kuua watu wetu zaidi ya watatu katika Kijiji cha Kahunda" amesema Athumani Wambura
Kwa upande wake Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho Kwa ushirikiano walioutoa mpaka kufanikisha zoezi la kumdhibiti mamba huyo na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli zao Katika ziwa hilo pamoja na kuzingatia elimu inayotolewa na watalamu hao huku akiwahakikishia kuwa Serikali imetenga fedha Kwa ajili ya kuongeza vizimba viwili katika halmashauri ya Buchosa ili kupunguza changamoto ya wanyamapori hao.