Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesaidia utatuzi wa changamoto ya upungufu wa vyoo katika shule ya msingi Chamugasa iliyopo Kata ya Kalemela, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu baada ya kuchangia kiasi cha shilingi milioni saba.
Akizungumza Ijumaa Oktoba 18, 2024 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Meneja wa Kanda ya Ziwa (TBS) Bi. Happy Kanyeka amesema hatua hiyo ni sehemu ya shirika kuunga mkono jitihada za Serikali kutatua changamoto za kijamii.
“Tunarudisha kwa jamii kile tunachokipata, hatua hii ni sehemu ya kuwezesha juhudi na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunza” alisema Kanyeka.
Pia Kanyeka alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo kutambua bidhaa zilizothibitishwa na TBS sambamba na kusoma taarifa zinazopatikana katika bidhaa wanazonunua kwa mahitaji mbalimbali akisema; “ukitumwa dukani kununua soda, maji, madaftari na bidhaa nyingine hakikisha unakagua nembo ya TBS na kusoma taarifa zilizopo hususan muda wa mwisho wa matumizi”.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Redempta Missanga alitoa shukurani kwa TBS kwa kusaidia ujenzi wa vyoo shuleni hapo akisema bado shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1959 inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vyumba nane vya madarasa na madawati 200.
“Shule hii ina wanafunzi 678 (wasichana 345 na wavulana 333), waalimu nane (wanawake watano na wanaume watatu). Tunaomba wadau mbalimbali waendelee kusaidia jitihada zinazofanywa ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia” alisema Mwl. Missanga.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Elizabeth Mafayo, Editha Misana na Zainabu Kusekwa wameishukuru TBS kwa kuchangia ujenzi wa vyoo vipya ambavyo vimeondoa adha waliyokuwa nayo hapo awali.
“Tulikuwa na changamoto za upungufu wa vyoo, tunashukuru TBS wametusaidia kujenga vyoo vipya kwa sasa hakuna changamoto tena” alisema mwanafunzi Eliza Mafayo.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Rhobiri Chacha amesisitiza michango inayotolewa na wadau katika halmashauri hiyo kufanya kazi iliyokusudiwa ili kuwatia moyo ya kuendelea kusaidia tena.
“Nawapongeza kwa kusimamia vizuri msaada uliotolewa na TBS, tukisimamia vizuri tulichopewa na kazi ikaonekana, tunawapa moto wa kusaidia zaidi katika maeneo mengine” alisema Chacha.