Na Mwandishi Wetu, Manyara
WAZALISHAJI wahimizwa kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha ili waweze kuuza bidhaa zao nje ya soko la Afrika Mashariki na pia kunufaika na sera ya Local Content.
Rai hiyo imetolewa Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini, Mhadisi Joseph Ismail, kwenye maonesho yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) yanayofanyika mkoani Manyara kuanzia tarehe 20 hadi 30 Oktoba 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo; "Manyara kwa Ustawi wa Biashara na Uwekezaji," Mhandisi Ismail alisema TBS wanaingiaji kwenye uwekezaji kwa sababu wanawezesha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Aliwataka wazalisha kurasimisha biashara zao, kwani baada ya kupata nembo ya ubora wataweza kuuza bidhaa zao nje ya Afrika Mashariki .
Alitoa mfano akisema Manyara ni mkoa wa kimkakati una hoteli nyingi, lakini haziwezi kununua bidhaa zisizokuwa na nembo ya TBS.
"Kwa hiyo ili uweze kuuza kwenye hoteli hizo ni lazima uthibitishe ubora wa bidhaa zako. Wenye mahoteli kupitia Sera ya Local Content badala ya kwenda kununua bidhaa Arusha watanunua Manyara , lakini hawawezi kununua bidhaa Manyara ambazo hazijathibitishwa ubora wake na TBS," alisema Mhandisi Ismail.
Alisema TBS ni taasisi rafiki ambayo ipo karibu sana na wajasiriamali, ambapo Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali.
"Kwa hiyo Serikali kupitia TBS inatoa huduma hiyo ya kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali pasipo kulipia gharama zozote," alisema na kuongeza;
"Kuthibitisha kuna gharama , lakini Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia TBS inatoa huduma hizo bure, kwa hiyo natoa hamasa kwa wajasiriamali waje TBS waweze kuthibitisha bidhaa zao."
Alisema wakishapata nembo ya ubora itawasaidia kuuza bidhaa zao katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi . Aidha, aliwataka wajasiriamali kurasimisha biashara zao ziweze kuwasaidia kupata mikopo kwenye mabenki.
Social Plugin