Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TPA TANGA BILIONI 18 NDANI YA MIEZI 3

 

MENEJA wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha akizungumza waandishi wa habari ikiwa ni siku ya wiki ya huduma kwa wateja
Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha kushoto akimkabidhi zawadi Mwandishi Mwandamizi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mkoa wa Tanga Bertha Mwambela ikiwa ni wiki ya huduma kwa wateja mapema leo



Na Oscar Assenga, TANGA

MAMLAKA ya Bandari (TPA) Tanzania Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha miezi mitatu ya robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 wamekusanya Bilioni 18 zilizotokana na ujio wa meli 11 huku asilimia 44.4 ya mapato hayo yakitokana na Meli za Kampuni ya Sea Front Shipping Services kutumia Bandari ya Tanga.

Hayo yalisemwa leo na Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku ya wiki ya huduma kwa wateja ambapo alisema kwamba wanapenda kumshukuru mteja huyo mkubwa na wateja wengine ambao wanaitumia Bandari hiyo.

Alisema kwamba wataendelea kuwashukuru na kushirikiana nao ili wajue changaamoto zinazowakabili ili waweze kuzirekebisha na wahakikishe wanapata huduma bora ya kiwango cha juu kitachowawezeshaa kurudi tena na kupata huduma katika Bandari hiyo na kufikia kwenye lengo walilokusudia.

Akizungumzia kiwango cha shehena ambayo wameihudumia kwa kipindi hicho alisema waliweza kuhudumia shehena ya tani 333,718 na hivyo kuvuka lengo lao waliojiwekea kwa asilimia 17.8 walijiwekea la kuhudumia tani 283,290.

“Utaona ni jinsi gani tumefanikiwa na tusingeweza kufanikiwa bila kutoa huduma bora kwa wateja mwaka jana kwa kipindi cha miezi mitatu kama hii tuliweza kuhudumia tani 200,004 mwaka huu tumehudumia 333,718 utaona namna tumeweza kuvuka lengo ”Alisema

Awali akizungumza Mwakilishi wa Kampuni ya Maersk ofisi ya Tanga Salum Mgaya alisema huduma za bandari ya Tanga hivi sasa zimefanyiwa maboresho makubwa ya vifaa na rasilimali watu na teknolojia imeongezeka ufanisi mkubwa na meli zao zinapoingia zinahudumiwa kwa wakati na makasha ya wateja yanatolewa kwa wakati.

Alisema kwamba hivi sasa meli zinafunga gatini na kuhudumiwa masaa 24 na wamekwisha kuleta meli kubwa yenye kontena 1,000 na imehudumiwa ndani ya wastani wa siku tatu mpaka nne kulingana na vifaa vilivyokuwepo lakini maboresho yaliyofanyika yameongeza ufanisi Bandari ya Tanga.

Naye kwa upande wake Mwakilishi kutoka Kampuni ya Star rock Shipping Vitalis Mokiwa alisema walikuwa wanadili na meli za mafuta na sasa wanadili na meli za mizigo mbalimbali ikiwemo ya kontena na wanaishukuru serikali kwa kuwaboresha bandari ya Tanga.

Alisema kwa sababu mwanzo meli zilipokuwa zinakuja mizigo ilikuwa inashushwa mbali na gatini na hivyo wakijikuta waingia gharama mara mbili lakini sasa kutokana na maboresho ya ujenzi wa gati ambao umewezesha meli kufika gati.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com