TUMIENI MIFUMO RASMI KUHIFADHI FEDHA-PINDA

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akikata utepe kuzindua tawi la Benki ya CRDB katika kata ya Majimoto iliyopo halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi tarehe 1 Oktoba 2024. Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Mpimbwe mhe. Silas Ilumba na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Islamic benki ya CRDB Bw. Rashid Rashid.

***************

Na Mwandishi Wetu, MLELE

Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Geophrey Pinda amewataka wananchi kuhifadhi fedha zao katika mifumo rasmi ya kifedha kwa ajili ya usalama.

Mhe. Pinda amesema hayo tarehe 01 Oktoba 2024 katika hafla ya uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB katika kata ya Majimoto iliyopo halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi.

"Natambua baadhi yetu tumekuwa tukihifadhi fedha zetu majumbani na hivyo kujiweka katika hatari ya kuzipoteza kutokana na wizi au janga lolote linaloweza kujitokeza" amesema mhe. Pinda.

Akitolea mfano wa majanga yaliyotokea Manyara wakati wa maporomoko ya matope na mafuriko wilayani Rufiji, amesema katika majanga hayo mawili waliohifadhi pesa ndani waliingia kwenye umasikini ila kwa wale waliohifadhi Benki angalau walikuwa na uhakika wa kuendelea na mipango baada ya kupona madhila yaliyotokana na majanga hayo.

Amebainisha kuwa, uamuzi wa benki ya CRDB kuanzisha tawi katika kata ya Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele ni ishara ya kuunga mkono jitihada za serikali za kuwajumuisha Watanzania kwenye mfumo rasmi wa huduma za kifedha.

"Ni furaha kubwa kwetu sisi wana Mpimbwe kuona Benki yetu ya kizalendo ya CRDB ikifanyia kazi mahitaji ya wateja wake kwa kusogeza huduma zake karibu zaidi na Watanzania hata waliopo vijijini" amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo Cha Islamic Banking cha CRDB Bw. Rashid Rashid amesema, kuanzishwa kwa tawi hilo kutatoa fursa ya mikopo kwa watu wote kwa ile mikopo yenye riba na isiyo na riba kulingana na imani zao.

‘’Benki yetu itahakikisha haachwi mtu nyuma kutokana na kigezo chochote yaani ukiweza kufika unapata huduma, hii ni katika jitihada kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma pasipo kukwazika kutokana na imani’’ amesema Rashid.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akisalimiana na Mkuu wa Kitengo cha Islamic Benki cha CRDB Bw. Rashid Rashid alipowasili kata ya Majimoto kuzindua tawi la benki hiyo katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 1 Oktoba 2024.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya CRDB katika kata ya Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 1 Oktoba 2024.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post