Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT) kimepata Viongozi wapya, watakao kiongoza chuo hicho baada ya mwekezaji wa kwanza kushindwa.
Walioteuliwa kuongoza chuo hicho ni Mkuu wa Chuo, Dkt. Kyung Chul Kam, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Sung Soo Kim na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kuwasimika Uongozi huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia masuala ya mipango, Fedha na Utawala, Profesa John Mwita alisema sababu za kuchagua uongozi mpya ni Uongozi uliopita kushindwa kufanya kazi.
"Shinikizo kubwa lilitokana na Serikali kuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wa mwekezaji wa kwanza kuwekeza kwenye eneo hili ambalo lina ekari 150...na tangu chuo kimeanza rasmi 2012 mpaka sasa serikali ikaona kuna wasiwasi wa kuendelezwa kwa hiki chuo.
"Kwahiyo mwekezaji yule wa kwanza ikabidi atafute mwekezaji mpya ambaye ni CTS ambayo Kampuni kubwa ya Television kule nchini Korea. Kwahiyo jawa ndo wakaja kununua chuo na kila kitu," alisema Profesa Mwita.
Alisema Chuo hicho kimesajiliwa rasmi na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ina hadhi sawa na chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inatoa fani ya mambo ya biashara na Engineering.
Kwa upande wake aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mukandala ambaye pia amesimikwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, alisema bado kuna changamoto ya kuwa na vyuo vikuu vya kutosheleza kutokana na idadi kubwa ya vijana wanaohitaji elimu ya juu.
"Bado tuna changamoto ya kuwa na nafasi za kutosha kwa wanafunzi ambao wanahitaji kusoma vyuo vikuu, kwahiyo hawa wenzetu kutoka Korea Kusini wamejitolea kuanzisha chuo hapa.
"Mwekezaji wa kwanza hakuweza kuendesha vizuri kwahiyo amepatikana mwingine. Lengo kubwa ni kuhakikisha chuo kinakuwa na misingi mizuri, miundombinu ya kutosha, vifaa, karakana ili waweze kuchukua wanafunzi wengi katika fani mbalimbali," alisema na kuongeza kuwa:
"Kwasasa tuna fani chache lakini mani kubwa kutakuwa na mabadiliko hivyo nawakaribisha watu waje wajiunge na chuo hiki,".
Social Plugin