Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mila na desturi ni mfumo wa utamaduni wa mawazo, tabia, na desturi zinazopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika jamii fulani kwa kujumuisha sanaa, muziki, lugha, imani, chakula, mavazi, na mitindo ya maisha.
Katika jamii nyingi, utamaduni unachangia sana katika kujenga utambulisho wa watu na kuimarisha uhusiano ambapo kwa tamaduni za Kiafrika mara nyingi zina muunganiko wa mila na desturi zinazohusisha jamii, na matukio kama harusi ,jando na sherehe za mazishi .
Kwa mkoa wa Dodoma Mila na desturi hufanyika kulingana na msimu ambapo lengo kuu la makala hii ni kuzungumzia umuhimu wa jando na mfumo wake.
Inapofika kipindi cha msimu wa baridi(Mwezi wa sita)huwa ndio msimu mzuri kuwapeleka watoto jando kwa sababu majira ya mwaka wa baridi yanatoa msaada wa watoto kupona haraka,lakini pia ni msimu mzuri sababu vijana wengi wanakuwa wamefunga shule kutoka muhula wa nusu ya kwanza kwenda nusu ya pili ya mwaka.
Wakati huu huwa ni muhimu pia kwa kuwa ndio huwa muda pekee wa mavuno hivyo wenyeji wa mkoa huu hususani wa vijijini hupendelea kuwapeleka watoto wao jando kutokana na uwepo wa chakula kingi hasa ukizingatia jando huchukuliwa kama tukio la ukarimu.
Jando ni mila na utamaduni inayowaandaa vijana kuingia katika umri wa utu uzima ambapo kwa kawaida mtu anayepelekwa jando hufanyiwa tohara na kuanzia kufundishwa maadili, elimu, na malezi.
Shughuli hizi mara nyingi zinaongozwa na wazee wa jamii na zinaweza kujumuisha sherehe na mafunzo ya maisha.
Wazazi na walezi huwapeleka watoto jando wangali vijana wadogo kuanzia miaka 4 hadi 15,ili kuwaepusha na magonjwa na hali ya kutojiamini wakiwa na wenza wao wakati wa ukubwa wao , jando pia ni faida kubwa kiafya.
Ifahamike kuwa utamaduni huu ni wa makabila mengi nchini Tanzania wakiwemo wa Maasai japo makala hii inaangazia zaidi utamaduni wa kigogo.
Kabila hili (Wagogo)hubeba suala hili kama mila na desturi zao ambapo kabla Serikali na mashirika ya utu wa mwanamke kuingilia kati wanawake pia walikuwa wanafanyiwa utamaduni huu ambapo kwa sasa imebaki historia na sasa suala hili limebaki kuwa kwa ajili ya wanaume tu .
Kwa asili hawa watoto wanapopelekwa jando hujulikana kwa lugha ya kigogo kama "Wanyamuluzi"ambapo mtoto anapofanyiwa toraha hupelekwa porini na kukaa huko mpaka apone japo kuna wengine ambao hujengewa vibanda vya nyasi nje ya nyumba zao.
Binafsi ,mwanzoni sikuwahi kukubaliana na jambo hili kwani niliona kama ni unyanyasaji wa haki za binadamu hasa pale nilipokuwa nikiona watoto wanapakwa matope mwili mzima na kukaa nayo katika kipindi chote cha jando .
Lakini sasa naelewa kuwa jambo hili ni muhimu kwani linaenzi mila na desturi zilizoachwa na mababu zetu kwa sababu kiuhalisia kuna utofauti kabisa kwa watoto wanaopelekwa jando kimila na wale wanaopelekwa jando kisasa.
Hawa "Wanyamluzi" wakati wa jando hupakwa udongo mwilini kwa lengo la kujihifadhi na baridi ambapo hukaa nao kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye hufanyika sherehe ya kuogeshwa(Mara nyingi anaogeshwa na bibi kizee),ngozi yake inakuwa nyororo sana, kisha anapakwa mafuta ya siagi ya maziwa ya ng'ombe ambayo hayajachemshwa hapo anakuwa anang'aa, ngozi laini,ameshapona,anaitwa Mwinzalu.
Na katika hatua hii ya mwinzalu utakuta hata kama ulikuwa umezoeana nae ,anakuwa hataki tena mazoea na mtu anakuwa kijana rijali ,mwanaume wa shoka ambaye amefundishwa akili zote za kiutu uzima hana tena zile tabia za kudeka deka.
Hapa namaanisha kuwa hata kama alizoea kukaa kaa jikoni utaona anabadilika na kuachana na zile tabia za mtoto wa mama na anakuwa anapenda kuambatana na wanaume wenzake tu kujifunza uanaume.
Hii ni kutokana na kuwa Wanyamuluzi hawa wanapokuwa jando hupewa mafunzo mbalimbali lakini pia hutumia nyimbo na hadithi za kigogo kuelimishana na kukaa kwenye mstari.
Mzee mmoja wa kimila mkoani hapa Mbogoni Nyaulingo anaeleza kuwa wanyamuluzi wanapokuwa jando hupewa fimbo ndogo ngumu,Kazi yake ikiwa ni kupigwa sehemu za enka ya mguu pale ambapo wanakuwa wamekosea,ni kama sehemu ya adhabu.
“Ni kazi nzito sana kuwafundisha watoto wanapokuwa jando kwani wengine wanakuwa ni watoto wa mama ambapo hata akikosea hataki umuelekeze lakini kulingana na sheria zetu za kijadi ni lazima tumnyooshe ili anapokuwa tayari kuingia mtaani awe na adabu na utii kwa wakubwa na wadogo,”anasisitiza mzee huyu wa kimila.
Anaeleza, "Haya mambo ya utandawazi yanatuharibia watoto utakuta mtoto anakosea na ukimuadhibu wanasema ukiukaji wa haki za binadamu, hakuna haki ya kibinadamu bila kufuata mila na desturi zetu, na haya mambo ndo yanayozalisha wanaume wasio na maadili na kuwa na kizazi kinachozalisha watoto na kuwatelekeza wanawake kwa sababu ya kuogopa majukumu, "anaeleza
Subira Mahinyila anasema mtoto anapokuwa tayari amepata mafundisho yote anaogeshwa na anavalishwa kanga au kitenge kipya, na nguo mpya,anatembea na fimbo yake mtaani kama ishara ya kuhitimu mafunzo ya jando , hakuna kucheka na mwanamke, anakuwa amenuna, hadi apewe pesa au zawadi nyingne, ndiyo anaongea au kucheka.
“Siku hii huwa ni sherehe kubwa,na hapo kijana huwa tayari anaruhusiwa kuanza kuchunga ng'ombe wakubwa badala ya ndama na mbuzi japo kuwa Sasa zama zimebadilika,si lazima kupitia hatua zote hizo za kijadi,bali vijana wanaweza kupelekwa jando kwa njia za "kisasa" japo kwa sisi wazee wa kimila tunaona kuna umuhimu mkubwa wa kufanya hivyo ili kuwajenga kifikra watoto,”anasema
Mahinyila anafanua kuwa japo kuwa lengo ni kuimarisha afya ya mtoto lakini pia mtoto huyu lazima apewe mafundisho ya jinsi ya kuheshimu mila na tamaduni zilizowakuza babu zake .
“Ni aibu,hata baada ya miaka 50 ya Uhuru,bado kuna mambo yahusuyo afya tunasubiri kushauriwa ili tuweze kuyafanikisha, naomba jamii ya wagogo tuachane na uswahili wa kuiga mambo yasiyo faa ,tuwapeleke watoto jando kwa umri unaofaa, "anaeleza
Anashauri wazazi kuwapeleka watoto jando kwa umri unaofaa ambao mtoto mwenyewe anakuwa anajitambua na kuachana utamaduni ambao umeibuka wa wazazi kuwapeleka watoto wadogo hadi wa miezi sita.
" Hii ni aibu, tukubali kuiweka jamii yetu kwenye mstari hasa kwa kuwa tabaka la vijana limebadilika sana na kuwa na vitendo vya kuiga ambavyo vinaumiza utu wetu huku wenyewe wakisema kuwa wanaenda na wakati,’’anasisitiza.
Mwandishi wa Makala hii amezungumza pia na Mzee wa kimila Kasuga Masenha ambaye hutumiwa kuwafanyia tohara vijana wa kiume ambaye anaeleza kuwa kulingana na utamaduni wa kabila hili la wagogo lilivyo,watoto wanapopelekwa jando(yaani makumbi kwa lugha ya kigogo ) hukusanya watu wengi kwa muda wa mwezi mmoja na zaidi .
Anaeleza kuwa ili mtoto awe mwanaume rijali lazima apite jando na kueleza kuwa ndiyo maana hata makabila ambayo hayakuwa na utamaduni huu kama wasukuma sasa hivi wanawapeleka watoto wao jando na wakati mwingine waliokuwa wamevuka kwenye kundi hili wanaanza kufanya tohara wakiwa watu wazima.
"Hii ni kutokana na kwamba kabila hili limeenzi ukarimu wa mababu hivyo baadhi ya familia huungana na kuwaweka watoto wao sehemu ambapo utakuta kumbi moja lina watoto kumi na kuendelea, " amefafanua.
Makumbi haya(Sehemu ambayo watoto waliofanyiwa tohara huwekwa) watu wengine hudiriki kusema kuwa ni hoteli za bure kwa kuwa chakula hupikwa na na kugawiwa bure kwa watu wote wanaokuja hapo.
Hakuna anayebisha kuwa watanzania ni wakarimu ,kila mtu anafahamu kuwa watanzania tumeumbiwa ukarimu tena ukarimu huu hata kwa watu tusiowajua.
Afisa Kilimo wa mkoa wa Dodoma Bernad Abraham anazungumzia suala hilo kuwa linapofanyika linapaswa kuzingatia kipato cha familia husika ili kuondokana na uhaba wa chakula
"Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya sehemu nilizotembea katika mkoa huu nimeshuhudia makundi ya watu wakishiriki katika sehemu hizo walizowekwa watoto kwa ajili ya mafunzo ya jadi yaani makumbi kwa lengo la kula chakula bila mpangilio na wengine hudiriki hata kumwaga au kuwapa kuku chakula kinapobaki, "anafafanua na kuongeza;.
Jambo la ajabu na la kusikitisha baada ya kuwaogesha watoto familia hizi zinaanza kulalamika njaa yaani chakula chote kimeisha kipindi walichokuwa wamewapeleka watoto jando, " anasema.
Ili kuliweka sawa jambo hili anasema ni lazima jamii ikubali kuwekeza kwenye kilimo ili kuendana na mahitaji yao .
“Natambua kuwa wagogo ni wakarimu sana hivyo ili kuundeleza ukarimu huu ni lazima wakubali kulima kwa kutumia kilimo cha kisasa ili wapate mazao mengi zaidi kuweza kukidhi jamii yao kwa kwa ujumla hasa pale wanapokuwa na sherehe za kimila kama hizo za jando,” anasema Afisa kilimo huyo.
Hata hivyo Abraham anasisitiza kuwa Jando ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao wanahama toka rika ya watoto kuwa watu wazima hivyo ili kumaliza manung’uniko ya uhaba wa chakula lazima vijana hawa badala ya kupelekwa porini kufundwa waelimishwe kwa vitendo suala zima la kilimo hususani cha umwagiliaji.
Social Plugin