Vijana nchini wametakiwa kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa kujiongezea ujuzi na kuwa wabobezi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na teknolojia hatua itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa Jumamosi Oktoba 12, 2024 kwenye kongamano la maadhimisho ya wiki ya vijana yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Oktoba 08-14, 2024 yakiwa na kaulimbiu isemayo “vijana na matumizi ya fursa za kidigitali kwa maendeleo endelevu”.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Imelda Banali alisema teknolojia pamoja na mitandao ya kijamii ni fursa kwa vijana ikiwa wataitumia kwa weledi.
“Ndiyo maana tumeanzisha klabu za kidigiti mashuleni ili kuwajengea uwezo wanafunzi kutambua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii lakini pia tunawezesha vijana kufanikisha mawazo bunifu” alisema Mhandisi Banali.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ubunifu ya Sahara Venture, Jumanne Mtambalike aliwaasa vijana kutumia vizuri rasilimali muda kwa kujifunza masuala mbalimali mtandaoni badala ya kumaliza muda na bando kwenye mambo yasiyo na tija.
“Hivi sasa kila kitu kiko mtandaoni, mfano ukiingia Youtube unaweza kujifunza masuala ya teknolojia, matumizi ya akili ‘Artificial Inteligence- AI (Akili Mnemba) na ukapata ujuzi wa kubadilisha kabisa maisha yako. Uamuzi ni wako, uingie Youtube kusikiliza muziki au fursa za mtandaoni na kukuza ujuzi wako” alisema Mtambalike akiwahimiza vijana kuwa na matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii.
Vijana kutoka maeneo mbalimbali walishiriki kongamano hilo wakiwemo wanafunzi kutoka shule ya sekondari Ibinza wilayani Ilemela ambao walikiri kuhamasika na elimu waliyoipata kupitia kongamano hilo.
“Nimejifunza kuchangamkia fursa mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kama vile kufuatilia matangazo muhimu ikiwemo nafasi za kazi. Lakini pia tunaweza kupata elimu ya matumizi ya AI ambayo ni muhimu kwa wakati huu dunia iko kidigitali” alisema Manyanda Alex.
Naye Mwalimu wa shule hiyo, Magreth Kitondo alitoa shukurani kwa shirika la KIVULINI kwa kuwezesha wanafunzi hao kushiriki kongamano hilo. Shirika hilo limekuwa likiwajengea uwezo wanafunzi kutimiza ndoto na malengo yao kitaaluma.
Maadhimisho ya wiki ya vijana yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Ijumaa Oktoba 11, 2024 katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza ambapo alitoa rai kwa mashirika yanayotoa elimu kwa vijana kuhakikisha hayakiuki maadili ya kitanzania.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali akitoa mada kwenye kongamano la wiki ya vijana 2024/
Mwanafunzi Jackson Manyama kutoka shule ya sekondari Ibinza wilayani Ilemela akichangia hoja kwenye kongamano hilo.
Vijana wakifuatilia kongamano hilo lililofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.
Waalimu na wanafunzi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Wanafunzi kutoka shule ya sekondari Ibinza wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kushiriki kongamano la wiki ya vijana.
Wanafunzi kutoka shule ya sekondari Ibinza wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kushiriki kongamano la wiki ya vijana.
Kongamano la vijana 2024 limeandaliwa na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) likiwa na kaulimbiu "vijana na matumizi ya fursa za kidigitali kwa maendeleo endelevu".
Tazama Video hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi