-BILIONI 16.7 KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 150
-KUNUFAISHA KAYA 4,950
Baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 785 Mkoani Mtwara, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 16.7 wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150 utakaonufaisha kaya 4,950 mkoani humo.
Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo Oktoba, 02, 2024 Wilayani Masasi Mkoani Mtwara mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Kanali Patrick Sawala wakati wa kumtambulisha Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd ya Arusha.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kukamilisha utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 785 mkoani hapa kwa asilimia 100 na sasa ni zamu ya vitongoji ambapo kiasi cha shilingi 16,717,407,821.65 kitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150,” alisema Mhandisi Nagu.
Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Nanyumbu, Mtwara na Tandahimba, Kamati za Usalama Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Masasi, Madiwani kutoka Kata mbalimbali Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala alizipongeza REA na TANESCO kwa kuendelea kushirikiana kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia Nishati linatimia.
“Wana Mtwara tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwani kwa sasa hapa kila Kijiji kina umeme na sasa wanahakikisha umeme unafika vitongojini,” alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme vitongojini, Mhandisi Nagu alisema kati ya vitongoji 3,427 vilivyopo Mkoani humo, vitongoji 2,200 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 64 na kwamba vitongoji 150 ambavyo vitapata umeme kupitia mradi huo vitaongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme katika Mkoa wa Mtwara.
Aidha, alibainisha kuwa mradi huo ambao mkandarasi wake ametambulishwa, utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na hivyo kukamilika ifikapo Septemba 2026 na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mhandisi Nagu alisema mradi utatekelezwa katika majimbo 10 katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu na kwamba katika kila Jimbo Vitongoji 15 vitanufaika.
“Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara ikiwa na lengo la kuwapatia huduma za Nishati wananchi ili kuboresha huduma za jamii maeneo ya vijijini na vijiji-miji,” alisema Mhandisi Nagu.
Kwa upande wake Mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd, Samwel Lema alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi utatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na utakamilika ndani ya muda kama ilivyo katika mkataba.
Social Plugin