Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA SEKTA YA MADINI WATEMBELEA BANDA LA TBS MAONESHO YA SABA YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA


Na Mwandishi Wetu, Geita

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekutana na wadau wa sekta ya madini na wananchi kwa ujumla na kuwapata elimu kuhusu masuala ya madini.

Shirika hilo limekutana na wadau pamoja na wananchi hao kuwapatia elimu hiyo kwenye Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita kuanzia Oktoba 02 ambapo yatafungwa Oktoba 13.

Maonesho hayo yalifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jana, Afisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema shirika hilo linaandaa viwango vya sekta ya madini, hivyo alisema kupitia maonesho hayo wanakutana na wadau wa sekta hiyo na kuwapa elimu.

Aidha, Mtemvu alisema mbali na kukutana na wadau wa sekta ya madini na wananchi kwa ujumla, kupitia maonesho hao wanakutana na wajasiriamali na kusikiliza na kutatua changamoto zao na kuwaelimisha na kuwahamasisha kuhusishana na umuhimu wa kuzalisha bidhaa zilizothibitishwa ubora na shirika hilo.

Mtemvu alisema shirika hilo litaendelea kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wajasiriamali wanashiriki katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango.

Alisema Serikali inatumia sh. milioni 250 kwa mwaka kugharamia gharama zote za wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha, hivyo wanapofika TBS wanapata huduma hiyo bure.

"Ndiyo maana tumetumia fursa hii na Maonesho ya Madini kuelimisha taratibu za kufuata ili kuwezakuthibitisha bidhaa zao bure," alisema Mtemvu.

Akifungua maonesho hayo ,Dkt. Biteko alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha, kuvutia na kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya madini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com