Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUNGWA 103 KUNUFAIKA NA MPANGO WA PAROLE




Na mwandishi wetu,Mwanza

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Balozi Khamisi Kagasheki, leo Oktoba 18,2024, amefunga kikao cha 51 kilichofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Aden Palace, Pasiasi, Jijini Mwanza.

Kikao hicho kimeridhia wafungwa 103 kunufaika na utaratibu wa parole baada ya kupokea maombi ya wafungwa 131 kutoka magereza 25, Tanzania bara.

Balozi Kagasheki, alieleza kwamba maombi hayo yalijadiliwa kwa kina kulingana na sheria na taratibu zilizopo, kuanzia ngazi ya Mkoa hadi kuwasilishwa kwenye Sekretalieti ya Taifa na hatimaye kwa Bodi ya Parole Taifa.

Aliongeza kuwa wajumbe wa Bodi hiyo walipitia na kuangalia vigezo vyote Kwa kina na kubaini wafungwa 103 wanakidhi vigezo kati ya 131 waliowasilisha maombi na 28 hawakupendekezwa kunufaika na parole.

 Mapendekezo hayo sasa yatapelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye akiridhia, majina yao yatatelemshwa ngazi za chini ili wahusika waweze kunufaika na mpango wa parole.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu alitoa ufafanuzi kuhusu maana ya parole, akisema, "Parole ni mpango wa kumruhusu mfungwa kutoka gerezani na kukamilisha kifungo chake akiwa uraiani kwa masharti ya kuwa na tabia njema."

CGP Katungu alisisitiza kuwa mchakato wa kuwapata wanufaika unaanzia ngazi ya gereza alilopo mfungwa, ambapo askari wa magereza wanaenda kufanya mahojiano na jamii ya mfungwa huyo ili kuthibitisha kama watamkubali kurudi kutoka gerezani. 

Aliongeza kuwa wafungwa ambao hawawezi kunufaika na utaratibu wa parole ni wale waliotenda makosa ya kujiusisha na biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, Ulawiti na vitendo vya kijinai.alieleza CGP Katungu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com