Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Dar es Salaam wameelezea kutofurahishwa na mwenendo wa viongozi wa chama hicho huku wakidai kusikitishwa na tabia iliyozuka karibuni ya vikao rasmi kufanyika nyumbani kwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.
"CHADEMA kwa sasa tuna ofisi tena za kisasa, jambo la kushangaza ni kuona vikao vya chama vinafanyikia nyumbani kwa Mwenyekiti Mbowe.
"Hivi vikao vina ajenda gani ya siri nyuma yake? Wafanye vikao ofisini, kisha sisi wanachama tupewe mrejesho.
"Vikao vya kimya kimya hivi havina afya kwa chama wala kwetu sisi wanachama. Ukiwa mwanademokrasia lazima uwazi wa mambo yanayoendelea ndani utawale,"amebainisha mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam ambaye amesema ni mwanachama mkubwa wa CHADEMA.
"Tena mimi ni mwanachama na kamanda mtiifu sana wa CHADEMA,Je ni sahihi kwa vikao vya CHADEMA kufanyika nyumbani kwa Mbowe?
"Au kuna Siri gani CHADEMA wanaficha hawataki kufanya vikao vya chama ofisini, vinafanyika nyumbani kwa Mbowe? Amehoji mkazi mwingine wa Ubungo jijini Dar es Salaam na mwanamama wa CHADEMA.
Hata hivyo, jitihada za kutaka kupata ufafanuzi kwa kina juu ya kile kinachodaiwa ni viongozi wa CHADEMA kuhamishia vikao vya chama nyumbani kwa Mheshimiwa Freeman Mbowe jijini Dar es Salaam bado zinaendelea.
Social Plugin