Wananchi wa maeneo ya Kibamba hadi Ubungo Jijini Dar es salaam wamekiri kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yao na kupunguza gharama kubwa za kuagiza huduma ya Majisafi kwa njia ya Magari takriban majuma machache yaliyopita.
Wakizungumza wakati wa zoezi la DAWASA la ufuatiliaji wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya kihuduma, Mwajuma Hussein mkazi wa Kimara mwisho amesema kuwa kwa sasa huduma imerejea na maji yanapatikana muda mrefu na kwa spidi nzuri.
"Kwakweli siku chache zilizopita tulikuwa na hali ngumu ya maji lakini sasa tangu juzi tunapata maji vizuri na tunaendelea kufurahia huduma ya maji". Ameeleza Mwajuma.
Naye Steven Jacob, mkazi wa Kibamba CCM ameishukuru DAWASA kwa jitihada zinazoendelea katika kuimarisha huduma ya maji katika eneo hilo.
"Hali ya maji imeanza kurudi vizuri, tulikuwa na mateso katika siku zilizopita lakini sasa maji yamefika na presha inaridhisha, tunawashukuru wataalamu wa DAWASA kwa harakati za usiku na mchana hadi kurejesha maji katika maeneo yetu."
Social Plugin