WAKULIMA KIJIJI CHA KINKWEMBE WAMUOMBA RAIS SAMIA KUINGILIA KATI SAKATA LA USHOROBA WA WANYAMA


Na Hamida Kamchalla, KILINDI.

ZAIDI ya kaya 300 za jamii ya wakulima katika kijiji cha Kinkwembe Wilayani Kilindi Mkoani Tanga zimemwangukia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zikimuomba kutengua amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo Hashim Mgandilwa aliyotoa ya kuwapa siku 14 kuondoka kwenye makazi yao bila kuwaambia eneo watakalokwenda na kuendelea kufanya shughuli zao za kilimo.


Wakizungumza na vyombo vya habari Mkoani Tanga wananchi hao wamesema kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi hapo wakifanya shughuli zao za kilimo lakini wameshangaa kupewa siku 14 kuondoka kwamadai kwamba eneo hilo ni Ushoroba wa wanyama.


Wakitoa kilio chao kwa Rais Samia wakulima hao wamesema wanashangaa kuona eneo hilo wakiambiwa ni ushoroba wa wanyama na kuamriwa waondoke wakati wenzao jamii ya wafugaji amri hiyo ikiwa haiwahusu na wakiendelea kutumia eneo hilo bila kubughudhiwa.

"Tunaomba mheshimiwa Rais atusikilize kilio chetu sisi hapa tayari tumefungua tawi tumejiandikisha kuwa wanachama halali wa ccm tuko zaidi ya wanachama 200 tayari tumeshaandikishwa usajili wetu umekamilika tunategemea kupiga kura hapa leo hii tunaambiwa ondokeni hatujui tunakwenda kupiga kura wala hatujui tunakwenda kuishi wapi familia sasa ivi zinateseka, "amesema Mathias Ernest mmoja wa wananchi hao.


Miongoni mwa wananchi hao akiwemo Halima Mmbelwa amesema kwa kipindi chote cha mwaka amekuwa akifanya shughuli zake za kilimo na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na baada ya agizo hilo hajui wapi atakapokwenda kuanzisha maisha mapya yatakayomsaidia kujikimu kimaisha yeye pamoja na familia yake.


Mwinjuma Sufian ambaye pia ni miongoni mwa wananchi hao amesema kufuatia agizo hilo hawatoweza kushiriki kwenye zoezi la upigaji wa kura na kwamba wamekiomba chama cha mapinduzi na serikali yake kuona jambo hilo kama changamoto ambayo wengi wai wanaweza kupigia kura vyama vingine vya siasa baada ya kukosa msaada kwenye chama wanachokifuata hivi sasa huku tawi lao likiwa halitambuliki.


Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa akiwa kwenye kijiji hicho aliwataka wakulima hao kuhama ndani ya siku 14 kwa madai kuwa eneo hilo ni ushoroba wa wanyama pori.

"Nawaomba wananchi wote ambao mmejenga hapa sio maeneo ya makazi hapa tayari yameshapangwa matumizi yake twendeni kijijini mkatafutiwe maeneo mengine kwahiyo mmeletwa na Kinkwembe rudini kijijini wawatafutie maeneo mengine umeletwa na Lengusero nenda kijijini wakutafutie maeneo mengine bado maeneo ya kuishi tunayo mengi sana, "alisisitiza Mgandilwa hivi karibuni.

Wananchi wa kijiji cha Kinkwembe Wilayani Kilindi Mkoani Tanga wanategemea shughuli za kilimo kama njia pekee ya kujikwamua kiuchumi na agizo la kuwataka kuhama walipo na kutafuta makazi mapya , wanaamini wanaweza kuathirika na kuanza maisha upya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post