EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameanzisha mpango mpya unaolenga kuwajumuisha watoto katika juhudi za kuripoti vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara kwenye jamii inayowazunguka.
Akizungumza leo Oktoba 16, 2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo hufanyika kila Jumatano kwenye Ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP, Dolice Alchard , amesisitiza umuhimu wa kuwapa watoto nafasi kupaza sauti katika kutafuta haki zao.
Aidha Dolice amesema kuwa mara nyingi wazazi wanaposhirikishwa katika masuala hayo, hawatoi ushirikiano wa kutosha, jambo linalosababisha ukatili kuendelea bila kutatuliwa.
“Tumekutana na changamoto ya wazazi kutoelewa umuhimu wa ushirikiano wao katika kuripoti vitendo vya kikatili,” amesema
Amesema ili kukabiliana na hali hii, mpango huo unajumuisha kuunda kamati mbalimbali za watoto, ambapo watoto watapata nafasi ya kupiga kura kuwachagua viongozi wao. "Kamati hizi zitaweza kusaidia watoto kujifunza uongozi na kujenga uwezo wa kujitawala".
Dolice ameeleza luwa, mchakato huo utaanza ndani ya familia ukilenga kuhamasisha ushirikiano wa wazazi na jamii. “Hatufanyi haya kwa mlengo wa kisiasa, bali tunalenga kusaidia jamii yetu,”
Pamoja na hayo amesema kamati hizo zitaweza kutoa mafunzo na ujuzi wa muhimu kwa watoto, ambao utaendelea kuwasaidia hata watakapokuwa watu wazima. “Ni muhimu watoto waelewe kuwa hawapaswi kusubiri serikali kufanya jambo fulani ili mambo yaende sawa,”
Ameeleza kwamba vitendo vya ukatili mara nyingi hutokea ndani ya familia ambapo baadhi ya watu hushindwa kutoa taarifa ili kumlinda mhalifu. “Ni muhimu kuhamasisha uwazi na uaminifu katika jamii ili kukomesha vitendo vya ukatili,” aliongeza.
Mpango huu wa GDSS unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuunda jamii inayojali haki za watoto na kupambana na ukatili wa kijinsia.
Social Plugin