WASIMAMIZI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 NGAZI YA KATA WAPATIWA MAFUNZO




Na Mariam Kagenda_Kagera

Wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake ,Vijana na watu wenye Ulemavu ngazi ya kata ambao ni Maafisa watendaji wa kata na Maafisa maendeleo ya Jamiii katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameanza kupatiwa mafunzo ambayo yanalenga kuwawezesha kupata ujuzi, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha usimamizi wa mikopo ya Vikundi vya Vijana , Wanawake na watu wenye Ulemavu .

Wakati akifungua Rasmi Mafunzo hayo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Bwana Jacob Nkwera amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tano ambapo watendaji wa kata watapata mafunzo hayo kwa siku 2 na maafisa maendeleo ya Jamii wa kata siku 3.

Bwana Nkwera amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuendeleza shughuli za vikundi vya Vijana,Wanawake na watu wenye Ulemavu hivyo ana imani kuwa watakuwa tayari kutekeleza jukumu hilo muhimu mara baada ya kupata mafunzo hayo
ameongeza kuwa Mikopo kwa Vikundi hivyo itatolewa kwa mujibu wa sheria ya fedha ya Serikali za mitaa Sura namba 290 kifungu cha 37A ambapo kifungu hicho kimefafanua kuwa mamlaka za serikali za mitaa zitakuwa na wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani yasiyolindwa ya mwaka husika kwa ajili ya vikundi hivyo ikiwa ni sehemu ya fedha zinazotengea kwa ajili ya Shughuli za maendeleo .

Kwa kuzingatia kifungu hicho halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 627 kwa ajili ya mikopo hiyo.ikumbukwe kuwa utoaji wa mikopo ya Vikundi vya Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu ilisitishwa April mwaka 2023 ili kufanya maboresho ambayo yanaweza kuweka urahisi wa utoaji wa mikopo hiyo na kwa sasa tayari Serikali imeboresha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo ili kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa mikopo na hivyo kutimiza hadhima ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza hali ya umaskini

Kwa upande wake mkuu wa idara ya maendeleo ya Jamii Manispaa ya Bukoba Bi Hellen Rocky amesema kuwa kwa sasa wasimamizi wa mikopo ngazi ya kata watakuwa ni watendaji wa kata ambao ni wenyeviti wa kamati za mikopo na maafisa maendeleo ya jamii ya kata watakuwa ni makatibu wa kamati ya mikopo ya kati  .

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kuweka utaratibu mzuri wa vikundi hivyo kupata mikopo ya asilimia 10 hasa ikiwa ni pamoja na kuweka wataalamu katika utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post