WAZIRI CHANA AZINDUA NEMBO YA ASALI YA TANZANIA



Na Happiness Shayo-TABORA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua nembo ya asali ya Tanzania itakayotumika kuitambulisha bidhaa hiyo katika soko la dunia huku akitoa rai kwa Wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kuuza asali nchini China.

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 4, 2024 katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) , Mkoani Tabora.

”Kupitia mradi wa BEVAC imeandaa nembo ya asali ya Tanzania (Tanzania Trade Mark). Uwepo wa nembo hii utawahakikishia walaji kuwa bidhaa watakayoitumia iko salama na inakidhi viwango vya ubora” Mhe. Chana amesisitiza.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Chana ametoa rai kwa wafanyabiashara wote wa asali ndani na nje ya nchi kuanza kuitumia nembo hiyo ya ubora huku akiielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – Tan Trade yenye jukumu la kusimamia matumizi ya nembo kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waweze kufahamu faida za matumizi ya nembo hii.
Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafugaji nyuki kwa kutenga maeneo maalum ya kufugia nyuki (Hifadhi za Nyuki); na kujenga viwanda nane (8) vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki katika Mikoa ya Tabora, Iringa, Katavi, Singida, Geita na Kigoma.

Vilevile amesema Serikali imeendelea kutafuta masoko mapya ya asali nje ya nchi, ambapo Julai 15, 2024 Tanzania imesaini Itifaki na nchi ya Jamhuri ya Watu wa China inayoruhusu asali ya Tanzania kuuzwa katika masoko ya China.

”Nitumie nafasi hii kuwataka wafanyabiashara wote wenye nia ya kuuza asali China kuwasiliana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ili kupewa utaratibu wa kuuza asali nchini China.” amesema Mhe. Chana.

Sambamba na hilo, Waziri Chana ameweka jiwe la msingi katika Jengo la bweni la wanafunzi wasichana la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora ambalo litagharimu Shilingi bilioni 2.65 sawa na Euro 954,314.4 na ujenzi wake utatumia muda ya miezi 12.

Amesema hatua hiyo inachochea ushiriki wa wasichana katika maendeleo ya sekta ya nyuki na kutumia fursa hiyo kutoa rai kwa wasichana kuchangamkia fursa hiyo na kujiunga na masomo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Mhe. Chana ameushukuru Umoja wa Ulaya Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki nchini na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL), Kituo cha Biashara cha Kimataifa ITC kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Tanzania inazalisha wastani wa tani 33,276 za asali na tani 1,913 za nta kwa mwaka. Kiwango hiki bado ni kidogo ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji wa asali ambao unakadiliwa kuwa tani 138,000 kwa mwaka. 

Hata hivyo, kiwango cha asali kinachozalishwa kwa sasa kinaiweka Tanzania katika nafasi ya 14 duniani, nafasi ya Pili Afrika na nafasi ya Kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post