Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO ATEMBELEA KIWANDA CHA LODHIA KINACHOTENGENEZA MABATI



Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia, Bw. Sailesh Pandit. Kiwanda hicho kinatengeneza mabati na kipo Kisanvule, Mkuranga (Pwani).
....

SERIKALI imetoa wiki tatu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka transfoma eneo la Mkuranga, mkoani Pwani kuviwezesha viwanda kuzalisha kwa urahisi.

Pia imewataka watumishi wa serikali kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji bali wawe msaada kufikia malengo yao, uwekezaji usonge mbele na kila mtu atimize wajibu wake.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo alipotembelea kiwanda cha Lodhia kinachotengeneza mabati kilichopo eneo la Kisanvule , Mkuranga kwa lengo la kuona shughuli zinazofanywa kiwandani hapo.

“Naomba uwekaji wa transfoma uwe umekamilika ndani ya wiki tatu, kuhakikisha dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na viwanda inakamilika,” alisema.

Akizungumzia uwekezaji wa kiwanda hicho, alisema jumla ya sh. bilioni 162 zimetumika kufunga mitambo hivyo wanapaswa kuanza uzalishaji.

Waziri Jafo alisema uwekezaji huo ni mkubwa kwani utaongeza pato la taifa na kupunguza tatizo la ajira.

“Nimeona baadhi ya changamoto ambayo serikali ikiweza kufanyia kazi viwanda hivi vitafanya uzallishaji na hiki kiwanda kipya kabisa kadhalika kitaanza uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Lodhia, Sailesh Pandit alisema kwa sasa kiwanda kimekamilika wanachokisubiri ni umeme waanze uzalishaji.

Alisema uzalisahaji utakapoanza wanatarajia kuzalisha tani 5,000 hadi 10,000 kwa mwezi hivyo aliwataka Watanzania kuviunga mkono viwanda vya ndani na kuondoa kasumba ya kupenda bidhaa za nje badala yake waone fahari kununua bidhaa inayotengezwa nchini.

“Watanzania tunatakiwa kusaidiana na kuona fahari ya kununua bidhaa inavyotengezwa nchini kwani kuna kasumba fulani yakuona bidhaa za nje ni bora kuliko za ndani. Lakini niwahakikishie bidhaa zetu zinakidhi ubora wa kimataifa.

“ Baada ya wiki tatu tunaanza uzalishaji wa mabati kama ambavyo Waziri amesema TRA wamekamilisha na kuruhusu transforma itolewe bandarini. Hapa tunasubiri TANESCO waje kufunga ili ‘supply’ ya umeme iwepo,” alisema.

Alisema soko lao litaanza ndani ya nchi na ukishakuwepo utoshelevu wanatarajia kwenda Afrika Mashariki, pia kiwanda hicho kwa sasa kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 620.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Ally alisema uwepo wa kiwanda hicho kutaongeza ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja na wilaya.

Alisema kiwanda kikianza uzalishaji wanatarajia kupata ushuru na mapato kupanda hivyo aliahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kuvutia wawekezaji wengi zaidi.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi.Hadija Ally wakati wa ziara ya kikazi katika kiwanda cha Lodhia .Kiwanda hicho kinatengeneza mabati na kipo Kisanvule, Mkuranga (Pwani).


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia, Bw. Sailesh Pandit. Kiwanda hicho kinatengeneza mabati na kipo Kisanvule, Mkuranga (Pwani).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com