Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA, ili waweze kuajiriwa au kujiajiri kwa urahisi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo juzi, tarehe 11 Oktoba 2024 alipokuwa akizindua Wiki ya Vijana Kitaifa katika uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza.
Amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa kwa vijana kupitia ujenzi wa vyuo vya VETA ambapo vyuo vipya 25 vimekamilika na vingine 65 vinajengwa katika kila wilaya na kwamba jukumu lililobaki ni la vijana kujiunga na mafunzo katika vyuo hivyo ili kujipatia ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas P. Katambi (MB) ameipongeza VETA kwa juhudi za kusaidia kukuza na kuendeleza ubunifu wa vijana.
Katambi ameyasema hayo alipotembelea banda la VETA kwenye maonesho hayo, tarehe 10 Oktoba 2024 na kujionea ubunifu mbalimbali wa wahitimu kutoka vyuo vya VETA nchini.
Kipekee, Mhe. Katambi amevutiwa zaidi na ubunifu wa mhitimu wa chuo cha VETA Mwanza, Benjamin Samweli ambaye ametengeneza gari linalotumia injini ya pikipiki lenye uwezo wa kubeba nusu tani, kutembea Kilometa 80 kwa saa, kutumia lita moja kwa Kilometa zaidi ya 20.
“Serikali katika Sera yake ya maendeleo ya vijana imeongelea kuwezesha vijana wenye uwezo na vipaji kuhusiana na ubunifu na uvumbuzi. VETA fuatilieni COSTECH kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kumsaidia mhitimu huyu kukuza na kuendeleza kipaji chake kwa kupatiwa mkopo nafuu ili aweze kuendeleza kipaji chake,” amesema.
Aidha ametoa wito kwa vijana kujiunga na Mafunzo na Elimu ya Ufundi Stadi ili kukuza uchumi wao kupitia ajira rasmi na zisizo rasmi.