Zaidi ya wananchi 900 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Pwani na mikoa mingine nchini wamefanyiwa huduma ya uchunguzi na matibabu ya macho bure inayofanyika katika Kituo cha Afya Chalinze kwa ushirikiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na Taasisi ya Vision Care ya Korea Kusini.
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka Muhimbili Mloganzila Dkt. Audrey Mwashilemo na kuongeza kuwa kati ya wagonjwa 900 waliofanyiwa uchunguzi na wagonjwa zaidi ya 90 wamefanyiwa upasuaji wa magonjwa mbalimbali ya macho ikiwemo kutoa mtoto wa jicho.
Dkt. Audrey ameongeza kuwa kuna baadhi ya wagonjwa wamekutwa na changamoto mbalimbali za uoni ambapo wamepatiwa matibabu, dawa pamoja na miwani kulingana na changamoto zinazowakabili.
“Tunawapongeza sana wananchi kwa kuitikia wito wa kujitokeza katika kambi hii, tumeshudia wananchi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Mbeya na Dar es Salaam wakiwa miongoni mwa wananchi waliokuja kupata huduma za uchunguzi na matibabu ikiwemo upasuaji wa magonjwa ya macho bure” amebainisha Dkt. Audrey.
Kwa upande wao wananchi waliojitokeza katika kambi hiyo wameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili, Vision Care pamoja na Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa kufanikisha matibabu yao bure na kuomba waendelee kuleta huduma kama hizi mara kwa mara kwa lengo la kuwatatulia changamoto za kufuata matibabu ya kibingwa mbali.
Zoezi hili la uchunguzi na matibabu ya macho bure limeenda sambamba na Siku ya Uoni Duniani ambayo huadhimishwa Jumatano ya pili ya mwezi Oktoba kila mwaka ambapo kauli mbiu mwaka huu ni “Yapende macho yako, mhamasishe mtoto kupenda macho yake”.