Tumbaku ikiingizwa katika moja ya maghala kwa ajili ya masoko.Picha na Robert Kakwesi
Viongozi na wakulima katika moja ya shamba la tumbaku Wilayani Sikonge.
Na Robert Kakwesi,Tabora
Tumbaku ni zao linaloingizia Taifa fedha nyingi za kigeni huku likitoa ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zipatazo 2.5 milioni.
Kupitia kilimo hicho na ajira hizo,wananchi wameingiza kipato na kupambana na umaskini huku wakiendesha maisha yao ikiwemo kujenga nyumba na kusomesha watoto wao.
Katika mwaka 2023/24, zao la tumbaku limeliingizia Taifa fedha za kigeni kiasi cha Dola za Kimarekani 494 milioni ambapo taarifa ya BOT ya mwezi Septemba 2023/24, ilionesha zao la tumbaku kuongoza kati ya mazao ya biashara kwa kulipatia Taifa fedha za kigeni huku miaka ya nyuma likipitwa na mazao ya Korosho na kahawa pekee
Katika msimu wa kilimo 2022/2023, wakulima wa tumbaku nchini wamelipwa shilingi 717 bilioni na shillingi 724bilioni kwa mwaka 2024 kiasi ambacho hakijawahi fikiwa tangu kilimo cha tumbaku kuanza kuzalishwa hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya Tumbaku,TTB,Stanley Mnozya,anaeleza kuwa msimu 2019/20, kampuni zilinunua tumbaku ya thamani ya Shilingi. 122.2bilioni na kulipa wakulima shilingi 121.3bilioni sawa na asilimia 99.3 ambapo Shilingi. 880milioni (0.7%) hazikulipwa huku msimu 2020/21, kampuni zikinunua tumbaku yenye thamani ya shilingi 208.1bilioni na zililipa wakulima kiasi cha Shilingi 203.3bilioni sawa na asilimia 97.6
Zao hilo limefanya uwepo wa ongezeko la makusanyo ya kodi mbalimbali za Serikali mpaka sasa imechangia zaidi ya Dola za Kimarekani 625.2million (Total Revenue) kwenye uchumi wa nchi, na mpaka mwisho wa msimu takribani Dola 763 Milioni zimekusanywa. Halmashauri za Wilaya zinazozalisha tumbaku zimeingiza zaidi ya shilingi 22 bilioni ikiwa ni ushuru wa zao kwa msimu wa kilimo 2022/23.
Kwa mujibu wa mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya tumbaku,TTB,Stanley Mnozya,kupatikana kwa kampuni mpya kumesaidia kufufua uzalishaji wa zao la tumbaku katika maeneo yaliyokuwa yamesitisha uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali. Maeneo hayo ni Mikoa ya Singida, Iringa,Kigoma, Geita, Kagera(Biharamulo), Mara (Serengeti) na Ruvuma pamoja na vyama vilivyokuwa vimesinzia katika mikoa ya Tabora, Mbeya, Shinyanga, Kigoma na Katavi
Anaeleza uwepo wa kampuni nyingi za tumbaku nchini zilizofikia 12, umesababisha ushindani katika sekta ndogo ya tumbaku kuongezeka, hali ambayo ni faida kwa mkulima na ukuaji wa Uchumi nchini, ambapo kumefanya kuongezeka kwa bei kutoka wastani wa Shilingi 3,255 kwa kilo katika msimu wa kilimo 2019/2020 hadi shilingi 5,825 msimu wa 2022/2023.
“Kuongezeka makampuni ya ununuzi wa tumbaku kutoka matatu hadi zaidi ya kumi,kumeleta ushindani mkubwa na wakulima kupata wastani mzuri wa bei ya tumbaku”Anasema
Anaeleza katika kipindi cha miaka mitano kuanzia msimu 2019/2020 hadi 2022/2023, uzalishaji umeongezeka kutoka kilo 37,550,753 msimu 2019/2020 hadi kilo 122,858,564 msimu wa kilimo 2022/2023 na kwamba uzalishaji ulishuka miaka mitano iliyopita baada ya wakulima kuzalisha kilo nyingi ambazo hazikununuliwa Katika miaka ya 2017/18, 2018/19 ambapo wakulima walizalisha kiasi kikubwa cha tumbaku na kukosa wanunuzi hali ilisababisha wakulima kuuza kwa hasara na kukata tamaa.
Mnozya anasema kutokana na jitihada kubwa za kuongeza wanunuzi wa tumbaku hali iliyosababisha kuongezeka ushindani, huku uzalishaji ukifikia kilo 122.8milioni msimu wa kilimo 2022/23,kuwa kumeifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kiuzalishaji barani Afrika, kutoka nafasi ya nne baada ya Zimbabwe ambayo imezalisha kilo 296milioni.
Anatamba kuwa Jitihada zinaendelea kuhakikisha inachukua nafasi ya kwanza kwa kuendelea kuwavutia wawekezaji wengi zaidi, kuimarisha masoko yaliyopo na kuwa na bei ambayo itaifanya tumbaku ya Tanzania kuweza kushindana katika soko la dunia.
Mnozya anabainisha kuwa msimu huu wa kilimo wa 2024/2025 ulioanza mwezi Machi 2024, kwa wanunuzi kutoa makisio ya awali ya ununuzi. Kwa kuzingatia mikataba ambayo imesainiwa baina ya wanunuzi na wakulima kupitia Vyama Vikuu, jumla ya kilo 226.2milioni za tumbaku, zinahitajika ,lengo alilosema litafikiwa kama hakutakuwa na changamoto zozote ikiwemo hali ya hewa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Japhael Lufungija,anaeleza kuwa zao la tumbaku ndio mkombozi kwenye halmashauri yake kutokana na kuingiza ushuru ambao unaifanya halmashauri hiyo kufanya vizuri katika makusanyo ya ndani na kutoa huduma kwa wananchi.
Anasema ushuru wa zao hilo unachangia zaidi ya asilimia sitini katika makusanyo ya mapato ya ndani na kufanya halmashauri kufanya vizuri katika makusanyo hayo ikiingiza kwa sasa zaidi ya shilingi bilioni 4 kutoka chini ya shilingi 1bilioni miaka tisa iliyopita.
“Mapato yetu ya ndani yanategemea sana ushuru wa zao la tumbaku,ambalo tunalipa kipaumbele sana huku tukiweka mazingira bora kwa wakulima wake”Anasema
Halmashauri hiyo iliyoanzishwa karibu miaka kumi iliyopita kutoka Wilaya ya Urambo,imeongeza uzalishaji kutoka kilo zipatazo 5milioni hadi zaidi ya kilo 22milioni msimu 2022/23 na 2023/24 na matarajio ni kuzidi kilo 30milioni msimu 2024/25
Zao hilo pia limeleta manufaa makubwa kwa wakulima wake kutokana na kulitumia kuendesha maisha yao ikiwemo kusomesha watoto,kujenga nyumba na shughuli zingine za kimaisha.
Mkulima Haruna Kasele wa kata ya Kazaroho,wilayani Kaliua,anasema kwa miaka mingi amekuwa akiendesha maisha yake kupitia zao hilo na kusomesha watoto wake,akijenga zaidi ya moja na shughuli kadhaa za kiuchumi.
“Nimeendesha maisha yangu kupitia zao hili ambalo nina utaalamu nalo kwa zaidi ya miaka ishirini sasa na likiwa limeendesha maisha yangu muda wote huo”Anasema
Said Ntahondi mkulima wa kata ya Isila,Wilayani Uyui,anaeleza kunufaika na zao hilo ambalo pia limemkutanisha na wakulima wengine nchini.
“Ni zao ambalo naliheshimu kwani mbali ya kuendesha maisha yangu kwa zaidi ya miaka kumi lakini pia limenipa jina wilayani Uyui na mkoa wa Tabora”anasema
Mkulima wa tumbaku Hamis Katabanya wa kata ya Ugunga,Wilayani Kaliua anayelima zaidi ya ekari 30,anasema zao hilo limempa heshima katika maisha yake,akiwa na usafiri na nyumba kadhaa pamoja na mifugo anayoitumia katika kilimo..
“Baada ya mambo kuwa mazuri,kwa kweli kwa sasa tunanufaika sana na zao hili na tumefanya makubwa na tutaendelea kufanya makubwa”Anaeleza
Festo Bwandu ambaye ni mkulima wa kijiji na kata ya Igagala,Wilayani Kaliua,anaeleza kuwa naye amenufaika na zao hilo baada ya kuwa katika hali nzuri tofauti na miaka kadhaa iliyopita ambapo hawakunufaika na zao hilo,akiwa amejenga nyumba ya kisasa na kununua gari sanjali na mifugo.
“Hili zao tumeanza kupata matunda yake miaka ya karibuni kwani miaka kadhaa iliyopita hali haikuwa nzuri kutokana na bei kuwa ndogo na uhakika wa kununuliwa pia haukuwepo”Anasema.
Mkulima mkubwa wa Tutuo,Wilayani SikongemAlbert Mtunda,anaeleza kuwa na ekari zaidi ya hamsini za tumbaku,akizalisha zaidi ya kilo laki mbili sanjali na kutoa ajira kwa waanchi wa Sikonge na nje ya Sikonge.
“Mbali ya kutoa ajira kwa wenzangu lakini pia nafuata kanuni bora za kilimo na utunzaji mazingira kwani lazima kutunza mazingira”Anasema
Hata hivyo mtunda kilio chake ni wakulima wakubwa kutambuliwa ili waweze kuwajibika wenyewe na sio kuwajibika kupitia kikundi au vyama vya msingi,akitaka wawajibike wenyewe hata kama ni kupitia vyama vya msingi lakini sio kama ilivyo sasa.
Wakulima pamoja na kupongeza uongozi wa bodi ya tumbaku,Wizara sanjali na Serikali kwa kusimamia ipasavyo zao hilo,wana maombi yao ikiwemo kulipwa kwa wakati pesa zao zote za malipo,kuongezwa kwa bei kwa kilo na pembejeo kupatikana kwa wakati.
Pia wanaahidi kufuata kutunza mazingira na kujitahidi kuendelea kujenga au kuwa na mabani ya kisasa ya kukaushia tumbaku ambayo yanatumia matawi ya miti na sio magogo.
Mkurugenzi mkuu wa bodi ya tumbaku,Stanley Mnozya,anasema watahakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati na makampuni ya ununuzi wa tumbaku na kwamba tayari wameanza na msimu uliomalizika kuna makampuni yamelipa wakulima ndani ya siku tatu au nne wakati muda uliowekwa ni siku kumi na nne tangu mauzo kufanyika.
Anasema wanafanya jitihada zaidi za kuongeza makampuni ili ushindani uongezeke zaidi sanjali na kutaka wastani wa bei kwa kilo nao uwe mzuri zaidi kwa lengo la kuwafanya wakulima wazidi kunufaika na zao hilo.
Hata hivyo wakati wakipigania hayo,anawataka wakulima nao wafanye kwa upande wao kwa kuhakikisha wanapanda miti kikamilifu na kuitunza,kutumia mabani ya kisasa yasiyotumia magogo,kutunza mazingira na kufuata kanuni bora za kilimo cha tumbaku.
“Tunataka kulifanya zao la tumbaku kuwa mkombozi kwa wakulima wake kiuchumi na kuingiza fedha nyingi zaidi za kigeni na hilo linawezekana kutokana na ushirikiano uliopo na Serikali kuamua zao hili kuwa mojawapo ya mazao ya kimkakati nchini”Anasema
Mnozya anasisitiza Bodi kutimiza wajibu sanjali na Serikali na kuahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili ili waendelee kunufaika na zao hilo ambalo linaingiza fedha nyingi za kigeni.
Kutokana na mipango iliyopo na utashi wa viongozi wa Serikali na kisiasa,ni wazi kuwa zao hili mbali ya kuendelea kuingiza fedha nyingi za kigeni lakini pia litaendelea kuwa mkombozi kwa wakulima wake na familia zao kwa kuwainua kiuchumi na kupambana na umaskini huku likitoa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja.