Na Mwandishi Wetu _ Malunde 1 blog
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Kimezindua rasmi Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Wilaya Kahama mkoani Shinyanga kwa kunadi Sera na Wagombea wa Chama hicho kwa Wananchi ili kuomba ridhaa ya Kuchaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 Mwaka huu.
Kampeni hizo zimezinduliwa leo Jumamosi Novemba 23,2024 na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu katika Viwanja vya Malori Manispaa ya Kahama,na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama hicho,ambapo amesema endapo Watapata ridhaa ya kuongoza Serikali za Vijiji,Mitaa na Vitongoji Watahakikisha Wananchi hawatozwi fedha za kupata huduma.
Amesema Wahakikisha Wananchi wanapata huduma bora katika Ofisi za Umma na Watakaokiuka Watawajibishwa,ikiwa ni pamoja kuondolewa katika Nafasi watakazokuwa nazo sambamba na kufukuzwa uanachama,kwani Viongozi hao Wanatakiwa kuwa faraja kwa Wanaowaongoza.
"CHADEMA endapo tukipewa Ridhaa tutahakikisha hakuna Mwananchi anayelipia Shilingi elfu 10000 ya Muhuri, katika Mtaa wake Huduma zitatolewa Bure,iwe unataka barua ya Dhamana,Mikopo au kwenda kuuza Mifugo hutatozwa chochote,niwaombe Wananchi jitokezeni kuwachagua Wagombea wetu ili tuunde serikali za mitaa,"amesema Mwalimu.
Sambamba na Hilo Mwalimu amesema CHADEMA haitojiondoa katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi huo kwa sababu inajua umuhimu wake na kuwataka Wagombea wa Chama hicho kuendelea na kampeni kuomba kura kwa Wananchi ili wapate ridhaa ya kuchaguliwa kuwa viongozi katika Maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi amesema endapo Wagombea wa Chama chake Watapata Ridhaa ya Kuchaguliwa Watahakikisha wanasimamia Rasilima za Nchi katika Mitaa yao ili zitumike kwa Manufaa ya Umma.
"Wenyeviti wa CHADEMA watakwenda kusimamia Ugawaji wa Ardhi kwa usawa,sehemu zenye Madini watahakikisha yanawanufaisha Jamii husika,na hawatakuwa sehemu ya Wala rushwa au hujuma katika usimamizi wa Rasimali hiyo Muhimu hapa nchini,"amesema Ntobi.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Serengeti , Lucas Ngoto amesema wamejipanga kufanya Kampeni za Kistaraabu na kuwaomba Wananchi kuchangua Wagombea wa chama hicho ambao wanawania Nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchanguzi huo.
"Kura ndio inaamua Mustakabali wa Maendeleo ya Mtaa, Kijiji, au Kitongoji,kwa kipindi cha miaka mitano,hivyo Wananchi hawana budi kuwachagua Wagombea wa CHADEMA katika Majimbo ya Kahama,Ushetu na Msalala ili waweze kuunda serikali zitakazokuwa suluhu ya Matatizo yao,"amesema Ngoto.