Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIOFARIKI AJALI YA KUDONDOKEWA GHOROFA KARIAKOO WAFIKIA 20, RAIS SAMIA AFIKA KARIAKOO


 
● Atangaza waliofariki wafikia 20, awatembelea majeruhi Muhimbili


Rais Samia Suluhu Hassan amewasili eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, ambapo jengo la ghorofa liliporomoka Jumamosi Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo vya watu wapatao 20 ambapo watu 80 wameokolewa.

Baada ya kuwasili eneo la tukio, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekagua jengo lililoporomoka kabla ya kuhutubia wananchi.

Rais Samia aliyekuwa nchini Brazil kwenye Mkutano wa G20 amewasili nchini na moja kwa moja kuelekea eneo lilipoporomoka jengo Kariakoo. 

“Jitihada zetu kubwa katika tukio hili ilikuwa kuwaokoa wenzetu walionasa ndani ya jengo hili wakiwa hai, ndilo lengo letu lililokuwa kubwa, lakini kama tunavyoambiwa jitihada haiondoshi kudra ya Mungu, pamoja na jitihada iliyofanywa na Serikali na waokoaji hawa walioko hapa lakini bado kuna wenzetu ambao tumewapoteza na taarifa niliyopewa leo ni kwamba mpaka saa tatu asubuhi tumepoteza wenzetu 20 ambao serikali imeshirikiana na familia kuwasitiri wenzetu ipasavyo,” amesema Rais Dkt. Samia.

Rais amekwenda kuwatembelea majeruhi watatu ambao wamelazwa Katika Taasisi ya Mifupa (MOI) Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu, mara tu baada ya kutoka eneo la ajali ya jengo Kariakoo.

“Hili sio pigo kwa familia zilizopoteza watu wao pekee yao ni pigo letu kama Watanzania na tunaguswa pia, ni kumbukumbu ya kutisha kwa wenzetu waliookoka hapa, kwa jinsi jengo lilivyo mtu akitoka hai bila shaka hawapo sawa (kisaikolojia), niombe wasifadhaike, wajipe moyo na tuendelee na shughuli zetu za kawaida bado Mungu ana kazi nao,” ameongeza.

Mama Samia amesema, tukio hili ukiangalia kwa macho tu lina viashiria vya kuwepo kwa mapungufu ya kiutendaji hivyo ametoe wito kila mtu atimize wajibu wake ipasavyo, na kwamba ukiangalia jengo hilo lilipewa vibali vya ujenzi kutoka Serikalini lakini jengo lile halikusimamiwa hivyo kukosa ubora wake wakati wa ujenzi.

Amewaomba wote wanaohusika Serikali Kuu, Halmashauri na Wananchi wote kwa ujumla kusema kwa pamoja kwamba matukio ya aina hii yasijirudie.

Rais ameagiza kufunguliwa kwa mitaa iliyofungwa ili wananchi waendelee kufanyabiashara zao kama kawaida, lakini eneo la tukio liendeleea kuzuiliwa kufungwa wakati wataalam wanaendelea kuwepo ili kuepusha hatari zaidi zinazoweza kutokea.

Dkt. Samia amewatahadharisha wananchi kuwa, mbali na jengo hilo kuwa ni hatari kwa usalama, pia linaweza kuendelea kuanguka na kuleta madhara zaidi.

Kwa lengo la kuzuia matukio kama haya siku zijazo, Rais Dkt. Samia amesema, akiwa nchini Brazil alimwagiza Waziri Mkuu kuunda Tume ya watu 20 ili kufanya ukaguzi wa majengo yote katika eneo la Kariakoo.

“Naambiwa Tume hiyo tayari imeundwa, baada ya kukamilisha kazi yao, tutazingatia mapendekezo yao, kama wataelekeza kwamba majengo yaliyo chini ya kiwango yabomolewe, hatutasita kuchukua hatua hiyo,” amesisitiza Rais Dkt.Samia.

Mbali na vifo vilivyoripotiwa, idadi ya majeruhi wa tukio hilo bado inaendelea kufanyiwa tathmini wakati timu za uokoaji, vikiwemo Vikosi vya Zimamoto, Polisi, na Wanajamii wa kujitolea, zimekuwa zikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usalama wa manusura na kurejesha hali ya kawaida katika eneo hilo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com