KISHAPU WALALAMIKIA UKOSEFU WA HUDUMA YA MAJI KWA SIKU 10, KIPINDUPINDU CHALIPUKA KATIKA KATA MBILI

 

Na Marco Maduhu,KISHAPU

Wananchi wa wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, wameeleza kutoridhishwa na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa kipindi cha siku 10, hali ambayo inahatarisha afya zao. 

Ukosefu huo umechangia kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu, ambapo kata mbili za Ngofila na Masanga zimeathirika kwa ugonjwa huo.
Diwani wa Kishapu Joel Ndettoson,ambaye ni mwakilishi wa wananchi, amesema sasa hivi kuna shida kubwa ya majisafi na salama wilayani Kishapu, ambapo mabomba hayatoi maji tena.

Diwani wa Kishapu, Joel Ndettoson, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wilayani Kishapu leo Novemba 6,2024 amesema hali ya maji wilayani humo ni mbaya na kuongeza kuwa tatizo la ukosefu wa maji limeshamiri katika kata tano. 

“Kuna shida kubwa ya maji, mabomba hayatoi maji na sasa tumeshaingia siku 10. Hali hii inatishia afya za wananchi, na tunaomba hatua zichukuliwe haraka,” amesema Ndettoson.
Meneja Wakala wa Maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)wilaya ya Kishapu Mhandisi Dickson Kamazima, amekiri kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa maji na kubainisha kwamba shida ipo kwa KASHWASA kwamba bomba la kupeleka maji wilayani humo ambalo lina matatizo ya presha katika sehemu ya kilomita moja ambapo mabomba hupasuka.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amesema kutokana na ukosefu wa maji wilayani humo, sababu ya bomba kuu la kupeleka maji kupasuka, alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa ili kutoa msukumo wa ukarabati wa bomba hilo,na kwamba jitihada zimefanyika ili kurejesha huduma hiyo ya maji.

Aidha,amesema ataunda timu ili kufanya uchunguzi wa kudhibiti tatizo la kupasuka kwa bomba la maji mara kwa mara tena eneo hilo hilo,na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji.
Ametoa pia tahadhari kwa wananchi, kwamba wazingatie kanuni za Afya ikiwamo kuchimba vyoo pamoja na kuvitumia, ili kukabiliana na mlipuko wa Kipindupindu, ambapo tayari Kata mbili za Ngofila na Masanga zimeshakumbwa na Kipindupindu,lakini tatizo hilo wamekabiliana nalo na ugonjwa huo umeisha.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akizungumza kwenye Baraza la Madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye Baraza hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu Emmanuel Johnson akizungumza kwenye Baraza hilo.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Kishapu Mhandisi Dickson Kamazima akitoa majibu ya kukatika kwa maji kwenye Baraza la Madiwani.
Baraza la Madiwani likiendelea wilayani Kishapu.

Madiwani wakiendelea na Baraza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post