Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia Tawi la Mwanza, imehimiza wananchi kukopa fedha kutoka kwa taasisi za huduma ndogo za kifedha ambazo zimepewa leseni rasmi na benki hiyo.
Hii ni kwa lengo la kuepuka mikopo isiyofaa, hasa inayohusisha riba kubwa, na kuwapa wananchi fursa ya kukopa kwa masharti bora.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 15,2024 jijini Mwanza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari Kanda ya Ziwa, Meneja Msaidizi Idara ya Uchumi kutoka BoT, Issa Pagali, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kutafuta huduma za kifedha kutoka kwa taasisi zinazozingatia sheria na zinazotoa mikopo yenye riba elekezi isiyozidi asilimia 3.5 kwa mwezi.
Pagali ameongeza kuwa BoT imekuwa ikitoa leseni kwa watoa huduma ndogo za kifedha na hadi sasa zaidi ya taasisi 2,100 zimepewa leseni.
Amesisitiza pia kuwa wananchi wanapaswa kutumia tovuti ya Benki Kuu kuangalia orodha ya taasisi zilizoidhinishwa, ili waweze kupata huduma za kifedha salama na zinazofaa.
Amesema, "Utoaji wa lesseni kwa watoa huduma ndogo za kifedha daraja la pili tumeshatoa lessen zaidi ya 2100 na maombi yapo mengi sana," na ameonya kuwa taasisi yoyote itakayokiuka masharti ya leseni, ikiwemo kutoza riba kubwa, itafutiwa leseni.
Pia, BoT inatarajia kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa kuelewa vigezo na masharti ya mikataba ya mikopo na kupata nakala ya mkataba uliosainiwa.
Kampeni ya Benki Kuu dhidi ya mikopo yenye madhara, inayojulikana kama "Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo," pia itaendelea kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza Gloria Mwaikambo.
Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza, Gloria Mwaikambo, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachunguza na kuangalia leseni za taasisi za kifedha wanazozitembelea, kwani leseni hizo hutolewa kwa uwazi na zinabandikwa ukutani kwenye ofisi za watoa huduma.
Amesisitiza umuhimu wa kusoma mikataba ya mikopo, kujua riba inayotolewa, na kuchukua nakala ya mikataba ili kuepuka matatizo ya baadaye.
Hii ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu kuimarisha mifumo ya mikopo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha kwa njia ya haki, uwazi, na kwa maslahi yao.
Social Plugin