Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Ruvuma zimeleta madhara makubwa kwa baadhi ya maeneo, ambapo nyumba 19 zimeezuliwa kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua hizo.
Madhara hayo yametokea Novemba 29, 2024, majira ya mchana, katika maeneo ya Mtaa wa Chandarua na Namanyigu, kata ya Mshangano, Manispaa ya Songea.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mvua hizo zimeathiri nyumba za wakazi wa maeneo hayo, na waathirika wa mvua hizo wamelazimika kutafuta maeneo mengine ya kujisitiri kutokana na uharibifu mkubwa wa mali zikiwemo nyumba zao.
"Ni pigo kubwa kwa wakazi wa maeneo haya. Nyumba nyingi zimeezuliwa na sehemu za kujisitiri sasa zimekuwa changamoto kwa wananchi," amesema mmoja wa viongozi wa mtaa wa Chandarua, akionyesha huzuni kwa madhara yaliyosababishwa na mvua na upepo huo.
Katika hatua ya haraka, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, ametembelea maeneo yaliyoathirika ili kutoa pole na faraja kwa waathirika.
Kapenjama amezungumza na baadhi ya wananchi wa maeneo hayo, akiwahakikishia kwamba Serikali pamoja na viongozi wa Mkoa na Manispaa wamesimama bega kwa bega na waathirika hao, na kwamba hatua za dharura zinaachukuliwa kusaidia wale walioathirika na maafa hayo.
"Tunaendelea kuwa na nia thabiti ya kusaidia waathirika hawa. Serikali iko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu, na tutahakikisha kuwa mnapata msaada wa haraka ili kurejea katika hali ya kawaida," amesema Mkuu wa Wilaya, Kapenjama Ndile.
Kwa upande wao, waathirika wa mvua na upepo kutoka Mtaa wa Chandarua wameishukuru serikali kwa kuwafikia haraka.
"Tulikuwa na hofu kubwa, lakini tunaishukuru Serikali kwa kutufikia haraka. Hatukutegemea kwamba nyumba zetu zingepata madhara haya tunaomba serikali itusaidie," amesema mmoja wa waathirika, akionyesha shukrani kwa juhudi za uongozi wa Wilaya.
Zaidi ya nyumba 19 zimeezuliwa, madhara mengine yaliyotokea ni pamoja na uharibifu wa mali na usumbufu mkubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Social Plugin