Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHAMIAJI HARAMU WAVAMIA SHINYANGA, JESHI LA POLISI LAKAMATA SABA, LATAKA USALAMA WAKATI WA UCHAGUZI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi

 Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kufanya doria na operesheni kubwa za kukabiliana na uhalifu na wahamiaji haramu, ambapo katika operesheni za hivi karibuni, wahamiaji haramu saba kutoka nchini Burundi wamekamatwa, hatua inayosemekana kuwa ni moja ya mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya uhamiaji haramu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Novemba 26,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema mnamo Novemba 13, 2024, wahamiaji watatu walikamatwa huko Kijiji cha Mseki, Kata ya Bulungwa, Wilaya ya Ushetu, wakiwa wameingia nchini kinyume cha sheria. 

Aidha, Novemba 17, 2024, wahamiaji wanne walikamatwa katika Kijiji cha Nyamilangano, Wilaya ya Ushetu, ambapo walikamatwa kwa kosa la kuingia nchini bila kibali cha mamlaka ya uhamiaji.

 "Wahamiaji wote saba ni raia wa Burundi na wamepelekwa katika ofisi za uhamiaji kwa hatua zaidi",amesema. 

Polisi Yakamata Wahalifu na Vifaa vya Wizi Kishapu

Huku operesheni za kudhibiti wahamiaji haramu zikiendelea, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga pia limefanikiwa kukamata wahalifu katika Wilaya ya Kishapu, wakituhumiwa kwa wizi wa mbegu za pamba na bidhaa zingine za Serikali.

Kamanda Magomi ameeleza kuwa Mnamo Novemba 15, 2024, huko Kijiji cha Mwamishoni, Kata ya Bubiki, Polisi walikamata gari moja aina ya Fuso lilikokuwa limebeba mbegu za pamba 210, ambapo mifuko 107 ya pamba iliibiwa kutoka katika chama cha AMCOSS Mwamishoni. Aidha, mnamo Novemba 23, 2024, mtuhumiwa mmoja alikamatwa huko Kijiji cha Maganzo kwa kuuza mbegu za pamba za ruzuku kwa mtu ambaye bado anatafutwa na Polisi.

Mafanikio Makubwa Katika Kudhibiti Uhalifu na Ulinzi Barabarani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema kuwa kuanzia Oktoba 24, 2024 hadi Novemba 25, 2024, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata jumla ya wahalifu 51 pamoja na vielelezo mbalimbali, vikiwemo Bhangi kilo 10, Pikipiki 09, Pombe ya moshi lita 15, Godoro 04, Container 02 za bati, Mashine 03 za Bonanza, Gari aina ya FUSO ikiwa na Nondo 130, Binding wire 11, Mifuko ya Saruji 100 vitu vinavyo dhaniwa kuwa vya wizi pamoja, Gari 01 aina ya Toyota Noah iliyotumika kubeba vitu vya wizi, Simu 02, Redio 07, Kabati 01, Fridge 01, na Kitanda 01 cha mbao.

Pia, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata makosa 7,920 ya uendeshaji wa magari na vyombo vya usafiri, ambapo wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa papo.

Katika upande wa kesi za uhalifu, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kuona hatua kubwa katika mfumo wa haki, ambapo washtakiwa kadhaa wamehukumiwa vifungo vizito. 

Kesi mbalimbali zimepata mafanikio, ikiwemo Mshtakiwa mmoja katika kesi ya kulawiti amepewa kifungo cha maisha jela, Washtakiwa watatu katika kesi za kubaka wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja na Washtakiwa wawili katika kesi za ukatili dhidi ya watoto na kusafirisha madawa ya kulevya wamehukumiwa kifungo cha miaka 5 kila mmoja.

Uhamasishaji wa Jamii na Usalama wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Kamanda Magomi amesisitiza umuhimu wa usalama katika uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa, akitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchaguzi na kwamba Polisi wamejipanga kuhakikisha usalama wa raia kutoka majumbani hadi kwenye vituo vya kupiga kura na kurudi majumbani kwao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com