Na Suzy Butondo,Shinyanga press Blog
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo amewataka wananchi wote wa kata ya Kambarage kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa viongozi wake wamefanya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii zikiwemo barabara na vituo vya afya.
Hayo ameyasema leo wakati akizindua kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika leo Novemba 21,2024 katika mtaa wa Majengo kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga
Batimayo amesema Chama Cha Mapinduzi CCM kwa usimamizi mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan kimefanya maendeleo makubwa katika Taifa la Tanzania na kwa kata ya Kambarage, barabara zilikuwa mbovu lakini kwa sasa zinapitika vizuri,kulikuwa hakuna kituo cha afya lakini kwa sasa kipo na wananchi wanapata huduma vizuri, wanawake wana uhakika wa kujifungua salama, hivyo tuendelee kuzaa tu kwa sababu usalama upo.
"Kinachotakiwa tutembee kifua mbele na tukawe mabalozi wa kuzungumzia maendeleo makubwa yaliyofanyika katika awamu ya sita,hivyo tupo katika kukumbushana na kuwaomba wananchi waendelee kutuamini kwani mama yetu mama Samia amefanya maendeleo makubwa na kama kuna mtu ambaye hayaoni maendeleo haya atakuwa na matatizo", amesema Batimayo.
"Na leo kazi kubwa ni kufanya uzinduzi kwa kuwaomba wananchi wachague wenyeviti na wajumbe wa kutoka CCM na si kwingine kwa sababu maendeleo tunayaona ambayo yalisimamiwa na wenyeviti wa CCM , hivyo tunaomba kura zenu zote kwa wenyeviti wetu na tunaamini watashinda kwa asilimia 100 , wapinzani waache kufanya majaribio kwenye maendeleo ya watu cha msingi tuchagueni mwenyekiti wa CCM", ameongeza
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole amesema toka mwaka 2000 walikuwa na shida ya ufaulu wa watoto lakini matokeo ya sasa wanafaulu vizuri na madarasa yapo ya kutosha, wote wataingia darasani hakuna atakayebaki.
Diwani viti maalumu Sheila Mshandete amesema katika kata ya Kambarage wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi kwa kwa kishindo, walikuwa na kero ya maji kuingia kwenye makazi ya wa watu lakini kwa sasa hayaingii tena, viongozi wa CCM wamelishughulikia.