Shirika la AKO Tanzania Community Support limeonyesha nia ya kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ili kuboresha utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya elimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa AKO, Bi. Hilda Kimath, alieleza dhamira hii alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, ofisini kwake Dodoma tarehe 8 Novemba 2024.
Bi. Kimath alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo ili kuongeza ufanisi katika miradi yao na kupunguza changamoto za gharama na ucheleweshaji.
‘‘Naamini tukitekeleza hii miradi kwa pamoja, tutakuwa na uhakika wa usimamizi lakini pia kuinua ubora wa miradi tunayotekeleza kwani TEA ambayo ni Shirika ni Serikali ina uzoefu wa kufanya miradi kama hii amesema” Bi Hilda
Dkt. Kipesha alieleza furaha yake kwa hatua hiyo na kupongeza juhudi za wadau kuchangia maendeleo ya elimu. Aliongeza kuwa TEA iko tayari kufanya kazi na wadau wote kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Alitaja faida za wadau kuchangia maendeleo kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ikiwemo kutambuliwa rasmi na kupewa Cheti cha Utambuzi, ambacho kinaweza kusaidia katika kupata nafuu ya kodi kutoka TRA.
TEA, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001, ina jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa ajili ya kugharamia miradi inayolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora na yenye usawa nchini.
Social Plugin