Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ameishukuru Umoja wa Afrika kwa kutoa kibali cha kuichangia nchi ya Tanzania Dola za Kimarekani 200,000 kama ishara ya mshikamano kutokana na maafa makubwa yaliyotokea Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara.
Waziri Lukuvi ametoa shukrani hizo leo tarehe 12 Novemba, 2024 katika Ofisi za Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu zilizopo Jijini Dodoma na kubainisha kuwa mchango huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia juhudi zinazofanywa na Serikali za kurejesha hali ikiwemo ujenzi wa shule, kituo cha afya na soko katika eneo lililoathirika.
Akipokea mchango wa fedha hizo kutoka kwa Mheshimiwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub Committee on refugees, Returnees and IDPs), Mhe. Lukuvi amemweleza kuwa, mwaka 2023/2024 Tanzania ilikumbwa na El-Niño ambayo ilisababisha kuwepo kwa mvua kubwa zilizofululiza kwa kipindi kirefu na kusababisha mafuriko, upepo mkali, maporomoko ya tope na udongo.
Ameeleza, pamoja na juhudi zilizofanywa na Serikali katika kuzuia na kupunguza madhara, bado El-Niño ilileta madhara makubwa ikiwemo maafa ambayo yaliyosababisha vifo, kuharibu makazi ya watu na miundombinu muhimu.
“Maporomoko ya tope wilayani Hanang’ yaliathiri maisha ya watu, miundombinu, shughuli za kiuchumi na kijamii, takwimu zinaonesha kuwa watu wapatao 89 walipoteza maisha na watu wapatao 139 waliumia kutokana na maporomoko hayo. Aidha, tathmini iliyofanyika inaonesha jumla ya nyumba 261 ziliathirika kwa namna moja au nyingine ambapo nyumba 95 zilibomoka kabisa na zingine kuzungukwa na tope, Watu wapatao 1576 kutoka 526 waliachwa bila makazi katika kipindi cha tukio” ameeleza Mhe. Lukuvi.
Aidha, ameongeza kuwa, katika kukabiliana na maafa, Serikali ilifanya juhudi za kurudisha hali ambapo mpaka sasa imewezesha kujengwa nyumba 108 za makazi ya watu, kati ya nyumba hizo 73 zimejengwa kwa fedha za Serikali na nyumba 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu, ujenzi wa nyumba hizo 108 umekamilika.
“Ninaelewa kuwa ujumbe wako utatembelea Wilaya ya Hanang’ tarehe 14 Novemba, 2024, katika safari yenu mtashuhudia juhudi kubwa za Serikali kwa kushirikiana na wadau zinazoendelea za kurejesha hali ikiwemo miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme, maji na ujenzi wa nyumba 108 za makazi, ameeleza Mhe. Lukuvi.
Kwa upande wake Mheshimiwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub Committee on refugees, Returnees and IDPs), ameeleza kuwa, ujumbe huo umeagizwa na Kamati ya Mabalozi kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea katika maeneo yaliyoathiriwa ikiwa dhamira kubwa ni Dodoma na Manyara, aidha muhimu zaidi ni kusikia kutoka kwenye mamlaka na ndio maana wamekutana na Mheshimiwa Waziri na timu yake.
“Muhimu zaidi kama Umoja wa Afrika kwa hakika kila kidogo tulicho nacho huwa tunainuka tunajivunia kuwa tumejitolea na kusema tunaenda kutafuta suluhu ya Afrika, matatizo au changamoto za Afrika” amebainisha Balozi Tabelelo.
Social Plugin