Uzinduzi rasmi wa kampeni hii unatarajiwa kufanyika tarehe 25 Novemba 2024 mkoani Manyara.
Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaya, amesema kuwa kampeni hii ni muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kushiriki katika kutokomeza vitendo vya unyanyasaji.
“Suala la unyanyasaji wa kijinsia ni la kimaendeleo, kwani linahusiana moja kwa moja na ustawi wa jamii na maendeleo endelevu,” amesisitiza Simbaya.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuelimisha jamii ili kufikia lengo la usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake na wasichana ifikapo mwaka 2030.
Kampeni hiyo itahusisha vyombo vya habari na majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile X (Twitter) na WhatsApp, ambapo wadau watakuwa na nafasi ya kujadiliana na kutafuta mbinu bora za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Hilda Kileo, Ofisa Programu na mratibu wa kampeni kutoka UTPC, amesema kuwa mkoa wa Manyara umechaguliwa kwa uzinduzi kutokana na kuongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, na kwamba kampeni hii itaimarisha uelewa wa jamii kuhusu madhara ya vitendo hivyo.
Kampeni ya siku 16 inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii na kuleta mabadiliko chanya katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Social Plugin