Bonanza la michezo la kuhamasisha ushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa lililoanza Novemba 23, 2024, na kuhitimishwa Novemba 24, 2024, limefanikiwa kuvutia umati mkubwa wa wananchi wilayani Kishapu.
Katika bonanza hili, timu ya Kishapu Veteran imeonyesha umahiri wake na kutwaa ushindi wa kwanza kwa kuifunga Kishapu Sekondari magoli 4-1.
Akizungumza kwenye hafla ya kufunga bonanza hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Bi. Fatma Mohamed, aliwashukuru wananchi kwa ushiriki wao mzuri na aliwasisitiza kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Amesema, "Ndugu zangu wananchi, mmelifanya bonanza hili kung'ara, hivyo wote mliofikisha umri wa miaka 18 na kuendelea na waliojiandikisha, tuhakikishe kuwa tarehe 27, 2024 tunaenda kwenye vituo vyetu elekezi kupiga kura na kuchagua viongozi watakaotuletea maendeleo katika taifa letu."
Bi. Fatma pia ametoa pongezi kwa timu zote zilizoshiriki katika michuano hiyo, akitaja Kishapu Veteran kama mshindi wa kwanza, Kishapu Sekondari kama mshindi wa pili, Igaga Combine kama mshindi wa tatu, na Bodaboda FC kama mshindi wa nne.
Amewatambua kwa kujitolea kwao na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata nafasi ya kutimiza haki yake ya kikatiba.
Zawadi kwa washindi zilikuwa ni pamoja na kikombe cha ubingwa, fedha za zawadi, mipira, na vyeti vya ushiriki.
Kishapu Veteran ameshinda zawadi ya Tsh. 150,000, mpira na cheti cha ushiriki, huku Kishapu Sekondari wakiibuka na Tsh. 100,000, mpira na cheti cha ushiriki. Washindi wa tatu na wa nne wamekabidhiwa mipira na vyeti.
Bonanza hili lilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, ambaye aliwashukuru wananchi kwa kuonyesha mshikamano na kujitolea kwa dhati katika kuhamasisha ushiriki wa uchaguzi.
Bonanza limehitimishwa kwa furaha na hamasa kubwa ya wananchi kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024
Social Plugin