Na Mbuke Shilagi Kagera.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mradi wa umeme wa maji ya maporomoko wa Rusumo umefikia asilimia 99.9 na kwamba ungewezekana kuzinduliwa mwezi wa 12 lakini kutokana na muda kuwa finyu kwa marais kushiriki katika uzinduzi huo watapeleka maombi ili ikiwezekana uzinduliwe mwezi Februari 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 15, 2024 katika kikao cha mawaziri wa nchi tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi ili kujiridhisha na mradi ulipofikia na lini utazinduliwa, Mwenyekiti wa wa kikao hicho cha Nchi tatu ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa nchi yetu inauhitaji mkubwa wa umeme ambapo mpaka kufikia Novemba 14,2024 kulikuwa na uhitaji wa megawati 1800 huku uwezo wetu wa kuzalisha ni megawati 3070 hivyo upo umeme wa ziada nchini.
Aidha Dkt. Biteko amesema kuwa nchi ya Tanzania inaendelea kukua kwa kasi kubwa katika ujenzi wa viwanda pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja ambapo katika mgawanyo wa matumizi ya kila siku asilimia 52 ni umeme majumbani na asilimia 48 ni umeme wa viwandani hivyo umeme unahitajika.
Sanjari na hayo amesema kuwa kutokana na mradi huo umeleta ajira kwa wananchi huku ukiongeza mahusiano baina ya nchi zote tatu na kwamba ili mradi udumu unatakiwa utunzwe kwa kulinda mazingira ambayo yamepitiwa na mradi kwa kuepuka kufanya shuguli za kibinadamu na kupanda miti ili kuendelea kuutunza mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amesema kuwa mradi huu ni fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika Mkoa wa Kagera kwasababu ni miongoni mwa Mkoa ambao hautakuwa na changamoto ya umeme huku akisema kuwa hata soko ni la uhakika kutokana na Mkoa kupakana na Nchi nyingine na katika ktunza mazingira Wana Kagera wamekuwa wakipanda miti na tayari katika Wilaya zote wanatekeleza azimio la Mh. Rais la kupanda miti milioni moja na laki tano kila mwaka.
Social Plugin