Na WAF, MWANZA
Hospitali tisa (9) za Halmashauri nane (8) za mkoa wa Mwanza zimepokea Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia wapatao 63 watakaofanya shughuli za kibingwa kwa siku sita (6).
Akiwapokea Madaktari hao Novemba 04, 2024 Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Bw. Elikana Balandya, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mpango huo unaogusa maisha ya watu ngazi ya msingi.
"Baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza ya kambi hizi Mhe. Rais ameona ni vema awatume tena, hivyo kwa niaba ya wananchi wa mkoa wetu sisi tunampongeza na kumshukuru sana Mhe Rais" amesema Bw. Balandya.
Bw.Balandya ameongeza kuwa zaidi ya milioni 2.6 kwa mwaka hujitokeza kwenye vituo mbali mbali vya kutolea huduma za afya na wengine hupewa rufaa kwenda kwenye hospitali za juu kwa ajili ya huduma bobezi hivyo ujio wa kambi hiyo ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kupata huduma kwa siku sita (6) zilizopangwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Afya ya Mtoto, Mtoto Mchanga na Vijana kutoka Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala, amesema uwepo wao kwenye huduma hizo tangu Septemba 9 mwaka huu wamehudumia wananchi 60,000 katika mikoa 20 na lengo ni kufikia mikoa yote 26 ndani ya wiki mbili zijazo.
"Zoezi hili litakamilika wiki ijayo, lengo letu ni kuona tunawafikia wananchi zaidi ya 80,000 tofauti na hapo awali ambapo tuliwafikia wananchi 70,000, hivyo nitoe wito wa Katibu Tawala kuwahamashishawananchi kujitokeza kwa wingi" amesema Dkt. Bundala.
Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba amesema zoezi la madaktari bingwa limekuwa kichocheo kikubwa cha ongezeko la makusanyo, kwani wananchi wanakuwa wamefikiwa kwenye maeneo yao na hivyo kujitokeza kwa wingi.
"Kama mkoa tuna upungufu mkubwa wa madaktari bingwa, niwaombe sana mkajitoe hata usiku mtakapohitajika kwani tuna uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa hasa Sengerema," amesema Dkt. Lebba.
Zoezi la madaktari bingwa limetajwa kuwa na faida nyingi ikiwemo kuwapatia ujuzi zaidi watumishi vituoni, uanzishwaji wa huduma mpya pamoja na kuimarisha baadhi ya miundombinu iliyokuwa imekaa bila kutumika.
Social Plugin