Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (Jimbo la Shinyanga Mjini) , Mwl. Alexius Kagunze
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (Jimbo la Shinyanga Mjini) , Mwl. Alexius Kagunze
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga yamekamilika kwa ufanisi mkubwa, na sasa kila kitu kipo tayari kwa ajili ya upigaji kura utakaofanyika kesho, Novemba 27, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26,2024 Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (Jimbo la Shinyanga Mjini) , Mwl. Alexius Kagunze, ameeleza kuwa hatua zote za maandalizi zimefanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya usimamizi wa uchaguzi, viongozi wa serikali, vyama vya siasa na jamii kwa ujumla.
Mwl. Kagunze amebainisha kuwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lilifanyika kwa mafanikio na kumalizika kwa wakati, na hivyo wananchi waliothibitishwa kuwa na haki ya kupiga kura wako tayari kushiriki kwenye uchaguzi.
Aidha, maandalizi ya vituo vya kupigia kura yamekamilika kwa asilimia 100, na Manispaa ya Shinyanga itakuwa na jumla ya vituo 285 vya kupigia kura.
"Wasimamizi wa uchaguzi wamejiandaa vizuri, na tayari wamechukua vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na karatasi za kupigia kura, vifaa vya usalama, na vifaa vingine vya kiutawala. Tuna uhakika kuwa uchaguzi utakuwa wa amani na utaratibu, na kila kitu kipo tayari kwa ajili ya upigaji kura," amesema Mwl. Kagunze.
Aidha amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia haki zao za msingi za kidemokrasia, kuchagua viongozi wanaowapenda na wanaowaona wanafaa kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2024 hadi 2029.
Mwl. Kagunze amesema uchaguzi huu unashirikisha vyama mbalimbali vya siasa, na kwamba vyama vilivyoweka wagombea wengi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo wagombea wao watashindania nafasi za uenyekiti na ujumbe katika mitaa, vijiji na vitongoji mbalimbali ndani ya Manispaa ya Shinyanga.
Mwl. Kagunze ametoa wito kwa wapiga kura kuhakikisha wanawahi vituoni mapema, kupiga kura kwa amani na utulivu, na kisha kuendelea na shughuli zao za kila siku huku wakisubiri matokeo ya uchaguzi.