RC MACHA : MSIWAFANANISHE WALENGWA WA TASAF NA WAFUNGWA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha kujenga uelewa kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga Wenyeviti wa Klabu za Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Tabora, Geita na Simiyu kuhusu utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini

Na Neema Paul - Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuhamasisha uelewa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, akionyesha wasiwasi kuhusu juhudi za baadhi ya watu kuharibu taswira ya mpango huo kwa kuhusianisha walengwa na wafungwa, jambo ambalo linapotosha hali halisi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi kikao kazi cha waandishi wa habari leo Novemba 7,2024 kilicholenga kutoa elimu na uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa walengwa wa mpango huo wanatekeleza kazi za mikono zinazosaidia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa walengwa wanapata kipato kutokana na kazi wanazozifanya, kama vile kuchimba mitaro na shughuli nyingine, na kwamba kumekuwepo na majaribio ya baadhi ya watu kupotosha picha za hali hii kwa kudai kuwa walengwa wanatelekezwa au kutendewa vibaya.

"Waandishi wa habari mtusaidie kuwaelimisha wananchi kuhusu tofauti kati ya wafungwa na walengwa wa mpango huu. Wafungwa wanatengwa na jamii kwa sababu ya makosa waliyoyatenda, lakini walengwa wa mpango huu wanajitahidi kwa kufanya kazi ambazo zinanufaisha jamii na taifa," amesema Macha.

Amesisitiza kuwa serikali imeanzisha mpango huu kwa nia njema, lengo kuu likiwa ni kuboresha hali za kiuchumi za kaya maskini na kuzipatia fursa za kujikwamua kimaisha.

Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendeleza juhudi za kuelimisha umma kuhusu faida na umuhimu wa mpango huo, ili kuepuka upotoshaji na kuendelea kuhakikisha kuwa taswira ya mpango inabaki kuwa chanya.


Kikao kazi hicho cha siku mbili kwa waandishi wa habari kwa waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga kilicholenga kutoa elimu na uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) pia kimehudhuriwa na Wenyeviti wa Klabu za Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Tabora, Geita na Simiyu.

Kikao hicho kimeandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) kwa ushirikiano na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post