Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa mafunzo kwa wahadhiri na wanafunzi kutoka vyuo vikuu na vyuo vya ufundi mkoani hapa yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya usajili wa bunifu mbalimbali.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika jijini hapa jana, Ofisa Usajili wa BRELA,Bw. Stanslaus Kigosi, alisema wanatoa elimu kuhusu miliki bunifu kwa sababu katika taasisi za elimu kuna tafiti na bunifu mbalimbali zinazofanyika, hivyo zinahitaji kulindwa.
"Tunatembelea vyuo hivyo kwa sababu katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vya ufundi, ndipo kunapatikana bunifu za kila aina ingawa hawatambui kwamba ubunifu huo ni mali inayopaswa kulindwa na kuwaingizia kipato," alisisitiza.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitengo cha Ujasiriamali na Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Dkt. Salum Matotola, aliishukuru BRELA kwa kutoa mafunzo hayo kwani wengi katika vyuo wanafanya tafiti mbalimbali lakini wanaishia kuyaweka matokeo husika katika maktaba badala ya kuwasilisha katika jamii.
"Ndiyo sababu tukaamua kushirikiana na BRELA kusaidia kufahamu haki zako zinaanzia wapi na zinaishia wapi, katika masuala ya haki bunifu kunawezesha tafiti hizo kwenda kwenye jamii kutatua changamoto na kuingiza kipato," alibainisha.
Mhadhiri kutoka UDOM, Dk. Benta Matunga, alieleza kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kufahamu namna BRELA inavyofanya shughuli zake ikiwemo hatua za usajili wa shughuli za kitafiti na bidhaa mbalimbali.
"Ninawafundisha wanafunzi wa mwaka wa tatu somo kuhusu kubuni wazo, hivyo itanisadia kuwafundisha umuhimu wa kusajili bunifu zao, hivyo nimeongeza uelewa mpana katika kusajili bunifu zao mbalimbali," alibainisha.
Naye, Mhitimu kutoka UDOM, Sospeter Jonathan, alisema alianza kujishughulisha katika masuala ya kiubunifu tangu akiwa mwaka wa kwanza wa masomo lakini hakuwa akifahamu kuhusu usajili wa miliki bunifu.
"Baada ya kufanya ubunifu kisha kufuata taratibu za kuisajili, nimeweza kupata manufaa mbalimbali ikiwemo kupata ufadhili kutoka COSTEC wa sh. milioni 19 ambapo sasa nipo tayari kuanza kuunda bidhaa yangu ambayo inaweza kuisadia jamii na kujiingizia kipato," alieleza.