Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejitokeza hadharani kukanusha vikali tuhuma zinazohusishwa nacho, hasa kuhusu madai ya rushwa na ufisadi yanayoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wake na yanayodaiwa kujitokeza ndani ya chama hususan katika chaguzi za ndani.
Taarifa hii imetolewa siku ya Alhamisi Novemba 14, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho John Mrema, ambapo amesisitiza kwamba Chadema iko mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ufisadi na rushwa.
“Tuhuma za Chadema kuwa na fedha chafu au rushwa ndani ya Chama au katika chaguzi za Chama. Tuhuma hizi zimekuwepo maeneo kadhaa, baadhi zimekosa vielelezo vya ushahidi wa kisheria na maeneo mengine bado uchunguzi wa ndani unaendelea”, ameeleza Mrema katika taarifa hiyo.
Mrema amesisitiza kuwa Chadema haijawahi kupokea wala kujadili madai ya rushwa, na kwamba kama kuna ushahidi wowote wa tuhuma hizo, unapaswa kuwasilishwa haraka kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika.
“Chadema imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi, ubadhirifu na rushwa miaka yake yote. Kama Chama kikiletewa ushahidi au vielelezo vya tuhuma hizo kutoka kwa mtu yeyote tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama dhidi ya Rushwa wa Mwaka 2012”, ameeleza Mrema.
Taarifa ya siku ya CHADEMA inajiri baada ya kuwa na malalamiko na taarifa za hapa na pale ambazo zimekuwa zikitolewa na wafuatiliaji wa siasa nchini Tanzania, wanachama wa chama hicho na viongozi wake wakubwa akiwamo Makamu Mwenyekiti wake Tanzania bara Tundu Lissu. Mjadala umebaki katika vinywa vya wengi juu ya athari ya shutuma hizo kwa chama hicho hasa wakati huu ambapo kinaelekea kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji Novemba 27, 2024.