DODOMA TUMEJIANDAA KUWAHUDUMIA ABIRIA WA SGR- RC SENYAMULE



Na. Hellen M. Minja,DODOMA RS

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, leo Novemba Mosi, 2024, amewapokea abiria 320 waliosafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa mara ya kwanza na treni ya SGR (mchongoko) katika stesheni ya Mkonze, Jijini Dodoma.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari punde baada ya kupokea treni hiyo, Mhe. Senyamule amesema;

“Abiria tuliowapokea leo ni 320, ndio mashuhuda wa kwanza kupanda treni hii inayokamilisha Dodoma kuwa na trip nne za kutoka na kuingia kila siku. Niwakaribishe Wanadodoma, lakini na Mikoa yote jirani inayotumia treni kupitia Dodoma, kwani tuna huduma nyingi na tumejiandaa kuwahudumia” Mhe. Senyamule.

Aidha Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa, uchumi wa Dodoma umekua na mabadiliko makubwa tangu kuanza kwa safari za treni za mwendo kasi kwa kuongeza mzunguko wa fedha kwa kiasi kikubwa.
“Sisi Mkoa wa Dodoma, tumeendelea kuona mabadiliko makubwa ya wanachi wakifurahia ongezeko la mapato kwani zaidi ya abiria 900 wanaondoka mara tatu kwa siku, ukiongeza na hawa wa mchongoko ni abiria 3,000 kwa siku. Kila mmoja anakua na hela hivyo katika kukaa kwao hapa wanachangia uchumi wa Dodoma”

Treni hiyo yenye madaraja mawili (Royal na Bussiness), inabeba abiria 583 kwa safari moja, inaongeza idadi ya safari kutoka mbili hadi nne kwa siku huku ikitumia takriban saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, na kufanya ratiba za safari kuwa; saa 11:15 Alfajiri, saa 08:10 mchana, saa 11:15 jioni na ya mwisho ni saa 12:40 jioni

Sambamba na mapokezi ya abiria, Mhe. Senyamule, amepata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo ya kutolea huduma yaliyopo ndani ya stesheni hiyo ya kisasa, ikiwa ni pamoja na sehemu ya kupumzikia wageni mashuhuri, eneo la kujiburudisha abiria wakati wakisubiri safari pamoja na mgahawa.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post