Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt John Kalage wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 20, 2024 katika Ofisi za HakiElimu Jijini Dar es Salaam.
**************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la HakiElimu Tanzania limeiomba Serikali kutengeneza mazingira yenye usawa kwa shule za michepuo yote ya Kiswahili na Kiingereza na kuondoa dhana potofu kwa wananchi na kwa viongozi kuwa shule za msingi za umma za Kiingereza, zina hadhi zaidi ya zile za mchepuo wa Kiswahili.
Hayo yameelezwa leo Novemba 20, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt John Kalage wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya taarifa ya kuwa Shule ya Msingi Ubungo National Housing inapandishwa hadhi' kuwa ya Shule ya umma ya mchepuo wa Kiingereza.
Amesema kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 lugha ya kufundishia kwa elimu ya msingi ni 'Kiswahili' isipokuwa kwa Shule ambazo zitaomba na kukubaliwa kufundisha kwa lugha ya 'Kiingereza'.
"Kwa mujibu wa Sera hii, lugha zote mbili zinabeba hadhi sawa katika utoaji wa elimu hapa nchini, sio kweli kwamba kwa shule kutumia lugha Kiingereza, Shule husika inakuwa 'na hadhi zaidi' ya zile mnazotumia lugha ya Kiswahili". Amesema Dkt. Kalage.
Amesema shule za umma za mchepuo wa Kiingereza zinaruhusiwa kutoza ada kutoka kwa wazazi kinyume na Sera ya utoaji elimu msingi bila ada, kwa mujibu wa taarifa ya uchambuzi wa HakiElimu, watoto hulipa ada kati ya 300,000 hadi 600,000.
Aidha amesema ada hizi zinafanya wazazi wenye kipato duni kulazimika kuwahamishia watoto wao kwenye kwenye shule za mchapuo wa Kiswahili ambazo baadhi yao ziko mbali na maeneo wanayoishi hivyo kuleta adha na kuongeza gharama kwa wazazi.
"Wasichana kutoka katika familia zenye hali duni ya kiuchumi wana uwezekano wa kuathirika zaidi, wanaposafiri umbali mrefu kuhudhuria masomo katika shule nymgine za umma za mchepuo wa Kiswahili, ikiwa ni pamoja na kutendewa vitendo vya ukatili vinavyoweza kusababisha kupata ujauzito pindi wawapo njiani kwenda na kurudi shule". Amesema
Meneja wa Miradi- HakiElimu, Godfrey Bonaventure akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 20, 2024 katika Ofisi za HakiElimu Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
Social Plugin