Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024 -Picha na Kadama Malunde
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka, kuisababishia serikali hasara, na kughushi nyaraka katika mradi wa ukarabati wa barabara ya Isoso – Mwabusiga, wilaya ya Kishapu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024 Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, ameeleza kuwa changamoto kubwa katika miradi ya barabara, hasa ile inayotekelezwa na wakandarasi, ni kutotekelezwa kwa viwango vinavyohitajika. Hii husababisha barabara kuharibika haraka baada ya matengenezo.
“Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, TAKUKURU ilifuatilia mradi wa ukarabati wa barabara za Isoso – Mwabusiga, Kishapu – Mwakipoya, na Gimagi – Magalata, miradi ambayo ilikuwa inafanywa na Kampuni ya Advance Construction Ltd chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Kishapu,” amesema Masanja.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi 206,214,500/=, ulijumuisha kipande cha barabara cha urefu wa kilometa 3 kutoka Isoso hadi Mwabusiga.
Amesema katika ufuatiliaji wa mradi, TAKUKURU iligundua kwamba mkandarasi alikosa kufanya baadhi ya kazi muhimu, ikiwa ni pamoja na ushindiliaji (compaction) wa kifusi cha barabara, jambo ambalo lilileta mapungufu katika ubora wa barabara hiyo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa, licha ya mkandarasi kulipwa kiasi cha fedha kilichokubalika katika mkataba, maelekezo ya TAKUKURU kwa meneja wa TARURA wilaya ya Kishapu ya kumsimamia mkandarasi kutekeleza marekebisho hayakutekelezwa.
“Tulielekeza meneja wa TARURA kuhakikisha mkandarasi anarekebisha mapungufu hayo, lakini maelekezo hayo hayakufanyiwa kazi. Hali hii ilitusababishia kuanzisha uchunguzi wa kina, ambapo tulibaini kuwa mkandarasi alilipwa kiasi cha shilingi 29,100,000/= bila kufanya kazi inayohitajika,” amesema Masanja.
"Uchunguzi wa TAKUKURU ulifunua pia kughushiwa kwa nyaraka za matokeo ya vipimo vya ubora wa ushindiliaji, ambapo nyaraka hizo zilikuwa zimeandaliwa na mhandisi wa mafunzo (Trainee Engineer) wa TANROADS Shinyanga, ambaye hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo",ameongeza Mwamba.
Amebainisha kuwa, baada ya uchunguzi, watuhumiwa watatu walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka, kuisababishia serikali hasara, na kughushi nyaraka. Watuhumiwa hao ni Mhandisi Juma Mkela, Msimamizi Mkuu wa Kampuni ya Advance Construction Ltd, Charles Emmanuel, Mhandisi wa Mafunzo wa TANROADS Shinyanga, na Mhandisi Wilfred Gutta, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu.
"Katika kesi hiyo, washtakiwa walikiri makossa yao na kutiwa hatiani. Mahakama ilitoa adhabu ya faini ya shilingi 500,000/= kwa kila kosa na kuamuru watuhumiwa kurejesha serikalini kiasi chote cha shilingi 29,100,000/= walicholipwa mkandarasi isivyo halali.
Watuhumiwa wote walilipa faini ya jumla ya shilingi 2,500,000/= na wamefanikiwa kurejesha shilingi 10,000,000/= kati ya shilingi 29,100,000/= wanazopaswa kurejesha. Aidha, washtakiwa wanaendelea na urejeshaji wa kiasi kilichobaki cha shilingi 19,100,000/= kama ilivyoamriwa na mahakama",amesema.
TAKUKURU inasisitiza kuwa itaendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma na kuzuia vitendo vya rushwa na udanganyifu katika utekelezaji wa miradi ya serikali.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024 . Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 13,2024
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Social Plugin